Kilo 798 za dawa za kulevya zanaswa Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:21 AM Dec 31 2024
Kamishna wa ZDCEA Kanal Nassoro Burhani
Picha:Mtandao
Kamishna wa ZDCEA Kanal Nassoro Burhani

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imefanya operesheni maalum za kimkakati na kufanikiwa kukamata kilogramu 798.893 za dawa za kulevya.

Dawa hizo ni aina ya bangi, cocaine, heroin, methampetamine na shisha zilizochanganywa na dawa za kulevya.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamishna wa ZDCEA Kanal Nassoro Burhani, alisema kiwango hicho kilichokamatwa ni kikubwa ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Zanzibar tangu Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964.

Alisema dawa hizo zingefanikiwa kuchepushwa na kuingia mtaani zinaweza kutengeneza kete milioni 27, wakati idadi ya watu wote Unguja na Pemba ni milioni 1.8 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Alisema katika operesheni hiyo gari sita, boti moja na watuhumiwa tisa kati yao nane ni raia wa Tanzania na mmoja ni raia wa kigeni, ambapo wote wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.

Alisema operesheni ya kwanza ilifanyika Oktoba 17 mwaka huu katika eneo la Bandari ya Majahazi Malindi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa wawili Haji Suleiman Ali (18) na Mbaraka Rajab Kiee (34) wakazi wa Maungani wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi gramu 734.95 zilizokuwa zimefichwa katika boti.

“Taarifa fiche zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa wanafanya biashara ya dawa za kulevya ndani ya eneo la Bandari ya Malindi katika maegesho ya majahazi. Aidha, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya upepelezi kukamilika”alisema.

Alisema operesheni ya pili ilifanyika Novemba 5, 2024, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ambapo walifanikiwa kukamata shisha boksi 15 sawa na pisi 300 zenye uzito wa kilogramu 263 zilizoingizwa nchini kutoka China na mtuhumiwa Alperen Karakurum raia wa Uturuki.

Aidha alisema baada ya kukamatwa kwa shisha hizo zilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kuwa ndani yake kuna kemikali mbalimbali ikiwemo ya “bufotenin” ambazo zinapumbaza akili ya mtumiaji na kusababisha athari mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa ya moyo.

Alisema operesheni ya tatu, ilifanyika Novemba 5, 2024 majira ya usiku, katika operesheni iliyofanyika eneo la Kilimani Chini na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Ali Mohamed Ali maarufu Ali Macho, mkazi wa Mpendae akiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa 87.223.

Aidha, katika eneo la Mtendeni walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Fahad Ali Khamis akiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 111.6678.

Alisema: “Operesheni ya nne, ilifanyika Novemba 15 katika eneo la Kisauni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi. Katika operesheni hiyo mamlaka imefanikiwa kuvuja rekodi yake ya mwezi Januari 2024, mara hii tumefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya methampetamine zenye uzito wa kilogramu 536 na heroin kilogramu moja zilizokuwa zimehifadhiwa katika nyumba iliyopo eneo la Kisauni”.