HaloPesa yatoa msaada kwa watoto wenye changamoto kichwa kikubwa

By Zuwena Shame , Nipashe
Published at 11:48 AM Oct 14 2024
HaloPesa yatoa msaada kwa watoto wenye changamoto kichwa kikubwa
Picha:Mpigapicha Wetu
HaloPesa yatoa msaada kwa watoto wenye changamoto kichwa kikubwa

KATIKA kusherehekea miaka minane tangu kuanzishwa kwake nchini, HaloPesa Tanzania imetoa misaada mbalimbali ya vyakula na mahitaji kwa watoto na wazazi katika taasisi ya Nyumba ya Matumaini ilichoko Kimara, mkoani Dar es Salaam.

Misaada imetolewa kwa wazazi/walezi na vijana wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Akizungumza kituoni huko jana, Kaimu Mkurugenzi wa HaloPesa, Magesa Wandwi alisema kuwa katika kuwajali wateja wao hasa watoto wenye uhitaji maalum, HaloPesa imeamua kuwapa faraja watoto na wazazi wa kituo kama njia moja ya kuonesha na kurudisha shukrani kwa jamii ya kitanzania.

Wandwi alisema Halopesa imeona uhitaji wa mahitaji ya wazazi na watoto hao kituoni huko, huku wakiwa wanasubiri matibabu.

"Kama HaloPesa, kuja kituoni hapa ni fursa kubwa kwetu. Na kama jamii tunahakikisha kuwa tunatumia mchango wetu kuendeleza ustawi wa watoto katika mazingira yao ya maisha ya kila siku," alisema Wandwi.

Alisema Halopesa inaamini kuwa watoto wenye uhitaji maalum ni kizazi na urithi wa Watanzania, hivyo kila taasisi ina jukumu la kuchangia watoto hao katika jamii.

"Kama jina la kituo linavyoitwa, 'Nyumba ya Matumaini', hivyo wazazi na watoto wa kituo hiki, wanahitaji faraja na misaada mbalimbali ili kupata matumaini na kujiona wao ni wanajamii, licha ya changamoto za magonjwa wanayopitia," alisema Wandwi.

Aliongeza kuwa kwa kutembelea kituo hicho, wafanyakazi wa HaloPesa wameona ni namna gani kila mmoja ana wajibu wa kushirikiana na wazazi na walezi wanaopitia changamoto mbalimbali kwa kupata wasaa wa kula chakula cha mchana na wazazi na watoto.

Mmoja ya wazazi wenye watoto wenye kichwa kikubwa kituoni huko, Fatuma Ali, aliishukuru Halopesa kwa kujua na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika kulea watoto hao, akiwaomba wadau wengine kuuiga mfano huo.

Fatuma alisema umoja huo wa wazazi na walezi kituoni huko, umewasaidia kuwa na sauti moja katika kutetea na kushawishi na kuweka maisha bora kwa watoto wao.

Alisema kuwa baadhi ya changamoto wanazopitia ni pamoja na kupata haki ya elimu, matibabu na mahitaji muhimu.