MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeutaja Mkoa wa Dodoma sasa unaongoza kwa matumizi ya dawa za kulevya, ikiwamo Heroine, ukifuatwa na Dar es Salaam.
Mei 17 mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2023, alisema Dar es Salaam ilikuwa inaongoza kwa matumizi na asilimia 78 ya watumiaji walikuwa vijana.
Kamishna wa DCEA, Peter Patric, aliiambia Nipashe siku chache zilizopita kwamba mikoa inayofuatia kwa kuwa na idadi kubwa ya matumizi ya dawa hizo ni Mwanza, Arusha na Mbeya.
Pia alisema dawa za kulevya zinazoongoza kwa kutumika zaidi nchini ni bangi, mirungi, heroin, cocaine na tiba zenye asili ya kulevya ambazo zinatumika pia hospitalini, licha ya kwamba baadhi huzitumia kama kilevi.
“Aina nyingine ni ‘methamphetamine’ ambazo tumeanza kuzikamata hivi karibuni na zilianza kuingia nchini kwa wingi mwaka 2021 na mwaka jana tulikamata zaidi ya tani mbili,” alisema Patrick.
Alisema asilimia 85 ya heroine inayotumika duniani inatoka Afghanistan na wanatarajia mwaka huu na ujao kiwango hicho kitashuka kwasababu Kundi la Talbani baada ya kuchukua madaraka na kuongoza eneo hilo wamepiga marufuku kilimo cha ‘Pop Plant’ ambalo ndio zao linalozalisha dawa hiyo.
“Hii dawa inakuja kwenye nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, kuanzia Somalia, Mombasa, Tanga, Mtwara, Lindi, Msumbiji mpaka Cape Town, kupitia Bahari ya Hindi kwa sababu zikizalishwa Afghanistan zinakwenda Iran au Pakistani.
“Tafiti zilizofanyika zinaonesha kwamba kati ya tani 50 mpaka 100 za dawa za kulevya aina ya heroine zinapita katika ukanda huu wa Mashariki na Afrika ya kati, lakini kiasi kinachotumika nchini ni chini ya tani 10,” alisema Patrick.
Aidha utafiti unaonesha kwamba karibu asilimia 36 ya watu wanaotumia dawa hizo kwa njia ya kujidunga wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Alisema wanawake wanaonekana kuathirika zaidi kwasababu utafiti unaonesha kati ya 100 wanaojidunga angalau 60 walikuwa wanaishi na VVU, na kwamba asilimia 90 ya tabaka hilo wanaotumia dawa za kulevya wanafanya biashara ya ngono ili waweze kupata fedha ya kununulia dawa.
Hata hivyo, alisema katika mamlaka hiyo wameweka mikakati mbalimbali ikiwamo kupunguza uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini,
Vile vile, wameweka mikakati ya kupunguza na kumaliza kabisa mahitaji ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yake ili umma usijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo.
“Mikakati hiyo pia ni kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini,” alisema Patrick.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED