DC Kigamboni apongeza upatikanaji huduma za nishati kwa wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:48 AM Oct 09 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo akisaini kitabu cha wageni kabla ya kuzindua kituo cha Nishati Safi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo akisaini kitabu cha wageni kabla ya kuzindua kituo cha Nishati Safi.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa jitihada zake za kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma na bidhaa za nishati kwa Watanzania kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Aliyasema hayo wakati aliposhiriki katika uzinduzi rasmi wa kituo kipya cha mafuta na huduma za ziada cha kampuni hiyo katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, Halmashauri ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 “Tanzania inashuhudia mapinduzi makubwa ya ukuaji wa uchumi wake na ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika, ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ni muhimu. Miongoni mwa sekta inayochochea ukuaji huu ni ya nishati, ambayo ni msingi katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Hivyo, kadri wananchi wanavyosogezewa huduma za nishati karibu hurahisisha upatikanaji wake na kuokoa gharama za kusafiri umbali mrefu,” alisema Bulembo.

Kituo kipya cha mafuta ambacho kinapatikana Dege Mtaa kitakuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani katika urahisishaji wa huduma za mafuta na bidhaa za vilainishi. Lakini pia kutakuwepo na huduma za ziada ambazo zitawarahisishia Watanzania wengi kufanya manunuzi ya mahitaji yao yote katika eneo moja kama vile duka la mahitaji mbalimbali ya nyumbani pamoja na kuwezeshwa kupata huduma za kununua na kujaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa gharama nafuu.

 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa dhamira yake ya kuendelea kusambaza huduma zake ili kuwafikia wananchi popote walipo, “jukumu la serikali ni kujenga miundombinu na kushirikiana na wadau kutoka sekta tofauti ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na maisha bora. Nawapongeza Puma Energy Tanzania kwa kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini,” aliongezea na kuhitimisha, “Ushirika huu unaendelea kuwanufaisha Watanzania kutokana kuwahakikishia upatikanaji wa huduma na bidhaa za nishati wa uhakika na gharama nafuu. Kama serikali, tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kuwahikikishia mazingira mazuri ya biashara ili muendelee kusambaza huduma zenu maeneo ya vijijini ambapo bado hawajafikiwa. Kwa niaba ya wakazi wa Kigamboni, tunawashukuru pia kwa msaada wa mitungi ya gesi ambayo itawanufaisha akina mama wanaojishughulisha na biashara ndogondogo ya uuzaji wa chakula ikiwa ni sehemu ya mkakati wenu mliojiwekea kuzisaidia jamii za Kitanzania ili kuchochea shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kote.”

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania na huduma za ziada katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, jijini Dar es Salaam. Akishirika pamoja naye kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah pamoja na Meneza Mauzo ya Rejareja (kulia), Sulpis Mmasi.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah alielezea kuwa uzinduzi wa kituo hiki sehemu ya mkakati wa kampuni kuendelea kuiwezesha jamii ya Watanzania na kuwahudumia wateja wake kwa ubunifu na weledi wa hali ya juu katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Dhamira yetu kuu ni kuendelea kuiwezesha jamii ya Watanzania pamoja na kuwahakikishia wateja wanapata huduma na bidhaa bora za nishati kwa gharama nafuu na kwa viwango vya hali ya juu. Hivyo, kama sehemu ya shamrashamra za Wiki ya Huduma kwa wateja sisi tumeona ni vema kufanya kwa vitendo kwa kuwasogezea huduma karibu zaidi. Uzinduzi wa kituo hiki kipya cha mafuta hautakuwa unatoa huduma za ujazaji wa mafuta pekee bali kutakuwa na huduma za ziada kama vile uoshaji wa magari, ufundi, mitungi ya gesi safi ya kupikia, vilainishi, pamoja na duka lenye mahitaji mbalimbali kwa matumizi ya nyumbani,” alifafanua Abdallah.

Wakazi wa Kigamboni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania alimalizia kwa kuwasihi wakazi wa Dege Mtaa kukitumia vema kituo hiko kipya ili kurahisisha shughuli za maisha yao ya kila siku. “Nawasihi wananchi wa Kigamboni kutumia fursa zitokanazo na uwepo wa kituo hiki kipya karibu na makazi yenu. Tunaishukuru serikali kwa ushirikiano endelevu na kututengenezea mazingira mazuri ya biashara ambayo yanatuwezesha kuendelea kusambaza na kuboresha huduma zetu. Kituo hiki kitakuwa kinatoa huduma masaa 24 kila siku kwa siku zote za wiki ili kuhakikisha watu hawakwami katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.”

Mbali na kuzindua kituo kipya cha mafuta na huduma za ziada, Puma Energy Tanzania ilikabidhi msaada wa mitungi 200 ya Puma Gas. Msaada huo uliokabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya unalenga kuwanufaisha wanawake wanaojihusisha na biashara ndogondogo za uuzaji wa chakula ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuiwezesha jamii ya Watanzania nchini kote.