Chalamila: Kwenye ulipaji kodi hakuna neno hiari

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:05 PM Oct 02 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza katika kongamano la kodi.
Picha Maulid Mmbaga.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza katika kongamano la kodi.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema katika mchakato wa ulipaji kodi hakuna neno hiari, akimaanisha kwamba kila mfanyabiashara anawajibu wa kulipa kodi na sio vinginevyo.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa kongamano la kodi 2024, ambalo limeandaliwa na taasisi ya OASIS ambao ni washauri wa kikodi, kwa lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema hakuna mtu ambaye anapenda kulipa kodi ndio maana zikawekwa sheria ili yoyote atakaeenda kinyume sheria hizo zitumike, huku akisisitiza kwamba hakuna njia yoyote kwa mfanya biashara kukwepa kulipa kodi.

"Mfanyabiashara yoyote anapoanza hajui kukwepa kodi lakini baada ya muda anajua, wafanyabiashara na TRA ni watu wenye mahusiano yasiyoisha. Na kunapokuwa na wimbi kubwa la ukwepaji kodi sisi tunakimbilia kupiga penati.

Mkurugenzi wa OASIS Stambuli Myovela.
"Ukiona kibaka kila siku anakuja kuiba kwenye nyumba yako, imarisha ulinzi. Hoja yangu ni kwamba ukiona wimbi ya ukwepaji kodi linakuwa kubwa, ndani kunasehemu kuna mianya ya kuruhusu hilo, hivyo TRA nendeni kuimarifa mifumo, ili mfanyabishara akiona aende kumuambia mwezie kule hakupitiki," amesema Chalamila.

Ameongeza kwa kusisitiza wafanyabiashara kufanya kazi kwa kuzingatia sera na kanuni za biashara kuliko kutegemea watu, akiwashukuru walioko Kariakoo kutotumia migomo kama njia ya kutafuta suluhu, na kwamba hatua zitakazochukuliwa zitasaidia kuwafanya walipe kodi bila kushurutishwa.

Aidha, amewashukuru TRA kwa kusaidia idadi ya walipakodi inaongezeka, pamoja na kiwango kinachokusanywa.

Naye, Mkurugenzi wa OASIS Stambuli Myovela, ambaye pia ni mtaalamu na mshauri wa masuala ya kikodi, alishauri TRA kupitia upya mifumo yake ili imsaidie mfanyabiashara kulipa kodi kwa urahisi.