CHADEMA mguu pande uchaguzi serikali za mitaa

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 05:49 PM Oct 02 2024
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara,Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara,Tundu Lissu.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutoa elimu ya kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Mitaa katika mamlaka za miji za mwaka 2024.

Aidha, kimewaambia wagombea wake kuwa wasipozijua kwa kina wataambulia patupu katika uchaguzi huo, huku chama hicho kikitaka kupata ushindi.

Leo Oktoba 2,2024 Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara,Tundu Lissu, ametoa mafunzo kwa viongozi na wanachama wa chama hicho wa Jimbo la Kibamba, Dar es Salaam  wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.

Mafunzo hayo  yalihusu mambo muhimu ya kuzingatia kwa wanaowania nafasi za uongozi, ikiwamo maelekezo yaliyopo katika  kanuni za uchaguzi huo na namna ya kujaza fomu za kugombea nafasi hizo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanachama wa chama wao ni kuongeza uelewa kuhusu masuala hayo na kuhamasisha wanachama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo.
Lissu amesema ni muhimu kufahamu kanuni hizo kwani bila ya kufahamu hawatoweza kushinda nafasi hizo kwa sababu zimesheheni mambo muhimu kuhusu uchaguzi huo.

Amesema wagombea wakifahamu kanuni hizo zitakuwa ni kinga wao juu ya mambo yoyote yanayoenda kinyume na uchaguzi kwani wakiona kitu chochote kinafanyika kinyume na kanuni hizo wana uwezo wa kukipinga.

“Waziri akitoa tangazo lake ili tujue lina uhalali kiasi gani tuanenda kuangalia kwenye msahafu huu. Utaratibu kwenye fomu za uchaguzi umewekwa humu, namna ya kujaza fomu, wakati wa kuzichukua, wakati wa kuzirejesha imeandikwa humu,” amesema.

Amewakumbusha pia kuwa makini wanapojaza fomu za kugombea nafasi katiika uchaguzi huo na kuhakikisha wadhamini wao pia wanafanya hivyo kwani wakizijaza tofauti watasababisha kukosa sifa za kugombea na chama kupoteza nafasi.

Amesema mwaka 2019 chama hicho hakikuwa na mwakilishi katika uongozi wa serikali za mitaa, hivyo katika mitaa yote nchini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipita bila kupingwa hicho chama hicho hakina uzoefu wa hivi karibuni wa uchaguzi huo.

Amesema matokeo ya mwaka 2004 ya serikali za mitaa kwa chama hicho katika jimbo hilo hayakuwa mazuri, na kwamba kati ya nafasi 44 za wenyeviti na 220 za wajumbe zilizokuwa zinashindaniwa chama hicho kiliambulia wenyeviti tisa na wajumbe 30.