JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) imelaani kitendo kilichofanywa na wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) cha kuchoma vitenge wanavyodai kupewa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku wakitaka vyombo vya dola viliache suala hilo washughulike nalo kisiasa.
Video imesambazwa katika mitandao ya kijamii ikionesha BAWACHA Kanda ya Pwani wakichoma vitenge vinavyodaiwa walipewa Siku ya Wanawake Duniani mwaka jana kwa madai Rais hajachukua hatua dhidi ya watekaji na wauaji wa kiongozi wa CHADEMA, Ali Kibao.
Alipotafutwa na Nipashe jana, Katibu wa BAWACHA Taifa, Catherine Ruge, alithibitisha kuchomwa vitenge walivyopewa kama zawadi na Rais ambavyo havikuwa na picha ya Rais na kwamba kinachoonekana ni kipande kimoja ambacho alipewa mwanamke ambaye ni kiongozi wa ULINGO aliyekuwa amealikwa kwenye kongamano la wanawake mwaka jana.
Akizungumza jana jijini Dodoma, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, alisema kitenge kimojawapo walichochoma kilitengenezwa na UWT Taifa ikiwa ni sare kwa ajili ya kongamano la kumpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri aliyofanya kwa kipindi cha miaka miwili, si kweli kwamba walipewa na Rais.
"Kongamano lililofanyika Machi 19, 2023 na toleo la kwanza la kitenge hicho lilitolewa tarehe Machi 13, 2023 hivyo ni uongo kusema kwamba Rais Samia ndio aliwagawia kitengo hicho kwa kuwa kwa tarehe iliyofanyika baraza lao kitenge kilikuwa hakijatengenezwa, bali wanachama wa BAWACHA walinunua kitenge hicho ikiwa ni sare kwa ajili ya kongamano la kumpongeza Rais Samia," alisema.
"Tuliwaalika na walihudhuria kwa wingi kitendo cha wana BAWACHA wengi kununua kitenge hicho na kuhudhuria kongamano letu ni kuashiria walikubaliana na ukweli kwamba Rais Samia ametekeleza mengi wa waliyoyaeleza kwenye Baraza Kuu la BAWACHA 8/3/2023. Wasiishie kuchoma vitenge, bali pia waeleze ukweli waliwezaje kufanya baraza hilo na wachome pia," alisema.
Alisema miongoni mwa hoja zao kuhusu Katiba Mpya, Rais alikubali kuendelea na mchakato na alisisitiza kuwa chama chake pia kimekubali, lakini lazima watanzania waelimishwe wajue Katiba ni nini na ni kitu gani na kinasemaje ndiyo wataweza kutoa mchango katika kutengeneza Katiba wanayoitaka kwa maendeleo ya taifa na asingependa suala la Katiba Mpya liwe takwa la wanasiasa.
"UWT pia hatuungi mkono matukio yanayotokea ya utekaji na mauaji mbalimbali nchini, tunalaani matukio hayo kwa nguvu zote. Bado tuna imani na vyombo vyetu vya usalama vinavyoendelea kuchukua hatua mbalimbali hapa nchini.
"Matukio haya yasiwe sababu ya kuvunja amani ya nchi yetu bali tuungane kama taifa kukemea na kusubiri uchunguzi wa vyombo," alisema.
Alitoa rai kwa vyombo vya dola kuhusu tukio la kuchoma vitenge waachane nalo, halina tija wala mvuto na watashughulika nalo kisiasa.
"Sisi UWT wanawake wenzao 'saizi' yetu, vyombo vya ulinzi na usalama visiwape promo, tunawaasa BAWACHA waache michezo ya kitoto, tushindane kwa hoja.
"Sisi UWT katu hatutochoma vitambara vyao maana hatuna kwa kuwa tuliona hatuna haja ya kuwa navyo kwa vile hawana mchango wowote katika taifa hili, tunaendelea kuwaonya kuwa watulizane, hiki kibiriti kina njiti na zinawaka, ninarudi wachezee ndevu, dola haichezewi," alisema.
Alisema Rais aliwathamini, aliwaheshimu na alitambua kuwa wote ni watanzania na kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi kwenye baraza lao mwaka jana.
Alisema kitendo hicho kiliingia katika historia dunia ya kuwa na Rais kutoka chama tawala kuhudhuria mkutano wa chama cha upinzani na tuzo waliyotoa kwake alistahili kutunukiwa.
Ruge, akitoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema, "Sisi tuligaiwa vitenge vya kawaida kama zawadi na Rais na havikuwa na nembo, ndivyo vilivyochomwa, pale kwenye video kinaonekana kitenge kimojawapo chenye picha ambacho kiongozi wa Ulingo, alipewa kwa ajili ya kongamano na hakukishona, alikuwa nacho, si kweli kwamba tulinunua, sisi hatuwezi kununua vitenge vya UWT."
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED