KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi amesema hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika kwa kuzingatia Takwimu zinazoonyesha kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria.
Dk. Yonazi amesema takwimu zinaonyesha kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndio kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 32 mwaka 2018 hadi 30, 2022.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 10 wa wadau wa lishe nchini ambao umefanyika leo Mwanza, na kuwakutanisha wadau wa afua za lishe.
"Lengo la mkutano huu ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa, na changamoto katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa tatu 2023/2024 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26)," amesema Dk. Yonazi.
Ameongeza kuwa mkutano huo unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Akiongelea kuhusu hali ya lishe amesema kiwango cha ukondefu pia kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi 3.5 mwaka 2018.
Dk. Yonazi amesema uwepo wa wadau katika mkutano huo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo na utayari wao katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania, hususan makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi.
“Naomba ushirikiano huo uendelee wakati wote wa utekelezaji wa mpango na hususan wakati kama huu ambao tunakutana kujadili utekelezaji sote tunajua kuwa ili tuweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni lazima Taifa liwe na watu wenye lishe na afya bora," amesema Dk. Yonazi.
"Hiyo pia ni ili kuwa na uwezo wa kufikiri, kutenda na kufanya kazi kwa bidii. Hivyo, juhudi hizi na nyingine ni muhimu kuwa endelevu ili kutuwezesha kufikia malengo,” amesisitiza Dk. Yonazi.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kuendelea kushiriki kikamilifu na kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha hali ya lishe kwa Watanzania inaendelea kuimarika.
Amesema serikali inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo na nyingine za wadau ili kuhakikisha taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED