Mama, binti wa kazi wanyongwa Tanga

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 06:58 PM Oct 02 2024
Nyumba ambayo tukio limetendeka.
Picha:Mtandao
Nyumba ambayo tukio limetendeka.

WATU wawili wameuwawa kwa kunyongwa na kamba kisha kutobolewa macho nyumbani kwao katika eneo la barabara ya nne jijini Tanga, huku baba mwenye nyumba Alii Mohamed Bagidad (60) hajulikani alipo.

Watu hao wamefahamika kama Saira Ali Mohammed (50) ambaye ni mama mwenye nyumba pamoja na binti wa kazi aliyetambulika kwa jina moja la Asha (20).

Nipashe limefika nyumbani kwa marehemu na kuzngumza na majirani wa familia hiyo ambao wamesema walikuta miili ya marehemu hao, ikiwa na kamba shingoni huku wakiwa wamewekwa nguo mdomoni. 

"Baada ya jirani mmoja kuja kugonga kwenye hii nyumba na kukuta ukimya alilazimika kuchungulia ndani ndipo akamuona mama mwenye nyumba yupo chini amelala na ikaonekana miguu ya msichana wa kazi.

"Lakini yule mama alivyokuwa akionekana pale chini alionekana kama amekufa ikabidi atafutwe mwenyekiti wa serikali za mitaa akasema haiwezekani kuvunja mlango itabidi tuwatafute polisi" amesema Halima Shebe ambaye ni jirani yake.

Shida huyo amebainisha kwamba baada ya polisi kufika walivunja mlango wa mbele na kuingia ndani akaonekana mama yuko kwenye korido wakaendelea mbele chumbani wakamkuta dada wa kazi naye amelala chini.

"Polisi walifanya taratibu zao za kutoa ile miili ya marehemu na kuiweka ndani ya gari, lakini mpaka sasa hatujui wale tukio wamefanyiwa na nani na baba mwenye nyumba mpaka saa izi anatafutwa hajulikani yuko wapi simu zake tangu jana hazipatikani kwahiyo hapa hatujui nani kafanya tukio hilo.

"Gari la baba mwenye nyumba lipo hapo nje tangu jana na yenye mwenyewe jana mpaka majira ya saa kumi jioni nimemuona, yaani bado tuna wasiwasi kufuatia jambo hili, nasubiria polisi wafanye kazi yao," ameongeza.