Raia wa Nigeria jela miaka tisa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:08 PM Oct 02 2024
Raia wa Nigeria jela miaka tisa
Picha: Mtandao
Raia wa Nigeria jela miaka tisa

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemuhukumu kifungo cha miaka tisa jela mfanyabiashara, Oje Boniface raia wa Nigeria na kuamuru nyumba, gari na fedha zitaifishwe na Serikali.

Hukumu hiyo ya Mahakama imesomwa leo mbele ya Jaji Godfrey Isaya baada ya mshtakiwa kupitia Wakili wake Lovenes Ngowi kukiri kosa.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Issaya amesema mshtakiwa aliingia maridhiano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya kukiri kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine jumla gramu 420.33.

"Kukiri kosa ni sehemu ya maridhiano, pande zote mbili ziliomba ziongozwe na mkataba wa maridhiano.

"Mahakama inabidi kufuata maridhiano, kwa kuwa sehemu ya makubaliano mshtakiwa atumikie kifungo cha miaka 12 badala ya miaka 30 au maisha na kwamba katika kutoa adhabu hiyo miaka mitatu aliyokaa ndani izingatiwe, Mahakama inapunguza miaka mitatu hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 9 jela,"amesema Jaji Isaya.

Aidha, amesema mahakama inatoa amri dawa za kulevya gramu 316.40 na gramu 103.93 ziharibiwe kwa kuchomwa moto.

"Kipande cha ardhi chenye nyumba iliyopo maeneo ya Mbezi Makabe, gari lenye namba ya usajili T414 DQF Toyota Premium zinataifishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,"amesema.

Jaji Isaya amesema mshtakiwa anatakiwa kuzingatia vigezo vyote vilivyopo katika mkataba na ana haki ya kukata rufani kwa adhabu peke yake.