Rais mpya MAT aanika vipaumbele vyake

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:55 AM Oct 02 2024
Rais wa MAT, Dk. Mugisha Nkoronko
Picha:Mtandao
Rais wa MAT, Dk. Mugisha Nkoronko

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesema kwa kipindi cha miaka miwili hadi 2026, kitajikita katika vipaumbele 10, ikiwamo kusimamia weledi na maadili ya wanatasnia hiyo.

Rais wa MAT, Dk. Mugisha Nkoronko, aliiambia Nipashe jana kuwa kipaumbele cha kwanza kwake ni kuendeleza ujenzi wa MAT kwa kusimamia weledi na maadili ya wanachama wake.

Alisema kipaumbele cha pili ni kuwaunganisha wanachama wote, wakubwa kwa wadogo, wa zamani na wa sasa, madaktari mabingwa wabobezi, ili kuunganisha nguvu za kupambana na adui maradhi kwa mtazamo wa kitaaluma.

Dk. Nkoronko alieleza kipaumbele cha tatu ni kuongeza ushirikiano baina ya taasisi kadhaa za ndani na nje ya sekta ya afya za ndani na nje ya nchi.

"Nne, nitaendeleza ushawishi na pengine kwa kutumia mbinu mtambuka na zilizothibitishwa kuleta matokeo makubwa sasa kwa serikali na wadau wa maendeleo kutunga sera na miongozo, inayozingatia maadili na weledi wa taaluma ya udaktari.

"Tano, nitasaidia na kuchangia jitahada za kukuza taaluma ya udaktari kuanzia ngazi za shule za udaktari na sita nitaongeza jitihada za kuelimisha wananchi, ili wajenge tabia njema ya kuzuia magonjwa, kuwahi hospitali wanapoumwa na kuchukua jitihada kwenye tiba za utengamao," alisema Dk. Nkoronko.

Alitaja kipaumbele cha saba kuwa ni kuwahamasisha madaktari kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na wa serikali kuu, mwaka huu na mwakani.

"Kipaumbele cha nane, nitahamasisha ushiriki wa wananchi na wadau wengine kwenye kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu na Agenda 2063 na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

"Tisa, pamoja na wadau wengine tutasaidiana kuongeza ushiriki wa madaktari kwenye shughuli za maendeleo, ili kuongeza mchango wa sekta kwenye  pato ghafi la taifa.

"Na mwisho, nitachagiza ushirikiano wa sekta binafsi, sekta ya umma na wadau wa maendeleo kujenga taifa lenye huduma bora za afya na zilizo salama," alisema.

Dk. Nkoronko anashika nafasi hiyo baada ya Dk. Deus Ndilanha, aliyeshika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.