NSSF yanuia kufikia theluthi ya Watanzania

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 09:32 AM Oct 02 2024
Baadhi ya wahariri ambao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewatambua kama watu wa mfano kwenye ustahimilivu kwa kutochukua michango yao hadi walipofika muda wa kustaafu kwa mujibu wa sheria, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee jana jijini DSM.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Baadhi ya wahariri ambao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewatambua kama watu wa mfano kwenye ustahimilivu kwa kutochukua michango yao hadi walipofika muda wa kustaafu kwa mujibu wa sheria, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee jana jijini DSM.

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umesema unatarajia kuandikisha wanachama milioni 21 kutoka sekta isiyo rasmi, huku umri wa kuchangia ukiwa ni kuanzia miaka 15 hadi 70 na kiwango kikianzia Sh. 30,000 na zaidi kwa mwezi.

Aidha, watu walio kwenye ajira wanaruhusiwa kuchangia michango yao kama namna nyingine (uchangiaji wa hiyari) ya kuweka akiba ya uzeeni kupitia mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mashomba, alikuwa akizungumza na wahariri wa habari kuhusu safari ya kuelekea kutoa huduma kwa sekta isiyo rasmi kwa kuwa na skimu maalum kwa ajili hiyo.

Katika kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani jana, NSSF ilitoa tuzo maalum kwa wahariri ambao wamekuwa wastahimilivu kwa kutochukua michango yao kwenye mfuko hadi walipotimiza kigezo cha umri kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii.

Pia ilitoa tuzo kwa waajiri wa sekta ya habari wanaopeleka michango ya wanachama wao kwa mujibu wa sheria bila kuchelewesha na ITV ilikuwa moja ya kampuni za habari zilizokidhi vigezo hivyo.

Akizungumza na wahariri, Mashomba alisema uchangiaji wa hiyari ni muhimu kwa walioajiriwa kwa kuwa unalengo la kuongeza akiba yake mtu atakapofikia umri wa kustaafu ambako mahitaji ni makubwa, na kwamba kuna wastaafu 30,000 wanaolipwa mafao ya Sh. bilioni 11.

Akiwasilisha mada ya safari ya kuelekea kutoa huduma kwa sekta isiyo rasmi, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omary Mziya, alisema sekta isiyo rasmi imeanzishwa kwa mujibu wa sheria kwa madhumuni ya kuhudumia wananchi waliojiajiri wenyewe katika shughuli za kiuchumi.

Alisema madhumuni ya kuanzisha skimu ni kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa makundi ambayo hayajafikiwa na huduma hizo ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa nchi, kusaidia juhudi za serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi, kuongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa nchi, na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mziya aliwataja wanufaika wa skimu hiyo kuwa ni mwananchi aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara ndogo, mama lishe/baba lishe, bodaboda, machinga na wanahabari wa kujitegemea.

Aidha, alisema mtazamo na malengo ya hifadhi ya jamii katika umri wa kufanyakazi ni kuhakikisha kila mtu anajiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya kujiwekea akiba ya uzeeni.

Aidha, alisema kukosekana kwa mipango mahususi ya Hifadhi ya Jamii katika umri wa kufanyakazi kunasababisha uwezekano wa watu wengi kuingia kwenye umaskini wa kipato katika umri wa uzee.

“Lengo la Hifadhi ya Jamii baada ya kustaafu ni kutoa kinga dhidi ya kushuka kwa kipato, kuhakikisha mstaafu anapata huduma zote muhimu ikiwamo chakula, malazi, mavazi na huduma za afya. Hali ya maisha baada ya kustaafu kutategemeana na jinsi ulivyojiandaa wakati ukiwa kwenye ajira. Maandalizi endelevu na ya uhakika ni kuwa kwenye mpango wa Hifadhi ya Jamii.

Alisema majukumu ya skimu ni kuelimisha wanachama, uandikishaji, kukusanya michango na kulipa mafao, huku vigezo vikiwa ni Mtanzania wa Tanzania Bara, mwenye umri wa miaka 15 hadi 70, asiwe ni mnufaika wa mafao ya pensheni kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini, awe na namna ya NIDA au kitambulisho chochote kinachomtambua (leseni ya udereva/ Mpigakura).

Alipoulizwa kuhusu vitambulisho na takwa la umri wa miaka 18 ndipo uvipate, alisema kwa ambao hawajatimiza umri huo watapokewa na kuunganishwa kwenye mfumo hadi watakapofikisha umri ndipo watatakiwa kuwa navyo kwa ajili ya kuwaunganisha kwenye mifumo.

“Kwa sasa vijana wadogo wanaanza kufanya kazi na kujiajiri tangu wakiwa na umri wa miaka 15, tumewawekea utaratibu kwa sababu tunajua wanakuwa hawajapata vitambulisho, ila wakishafikisha umri lazima wawe navyo kwa ajili ya kuwaunganisha kwenye mfumo,” alisema.

Kuhusu kiwango cha kuchangia, Mziya alisema kiwango cha michango ni Sh. 30,000 au zaidi kwa mwezi, na kwamba mwanachama anapaswa kutumia namba ya kumbukumbu (control number) kuwasilisha michango yake, na inaruhusiwa kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula au msimu.

Mziya alisema mwanachama anaweza kulipa michango kwenda mbele kwa muda wa miezi 12, ikiwa ameshindwa kulipia kila mwezi kutokana na chanzo cha kipato kuwa cha msimu, na kwamba akishindwa kulipa ataruhusiwa kuchangia michango kurudi nyuma kwa kipindi kisichozidi miezi 12.

Aidha, alisema michango ya kipindi kisichozidi miezi 12 kitakacholipwa hakitotozwa adhabu, huku mafao yatakayotolewa ni ya muda mrefu ya pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, ya muda mfupi ni uzazi, matibabu, kujitoa (sehemu ya michango isiyozidi asilimia 50 au malipo ya mkupuo ya michango yote) na msaada wa mazishi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu Mashomba alisema ukuaji wa sekta ya hifadhi ya jamii kwa waajiri na waajiriwa ni asilimia 70, huku msisitizo mkubwa ukiwa kwa sekta isiyo rasmi ili iweze kunufaika na huduma hiyo muhimu kwa maisha ya uzeeni.

Alisema NSSF imeboresha mifumo ya TEHAMA na hadi kufika Juni mwaka huu asilimia 80 ya huduma zote zitakuwa zinatolewa mtandaoni, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 40 miaka mitatu iliyopita.

“Wanachama wetu wengi walikuwa wanalazimika kuja kwenye ofisi zetu kupata huduma, sasa tumekuja na portal inayomwezesha mwanachama kuhudumiwa popote alipo kwa kupitia simu au kompyuta. Kwa sasa unaweza kuanza na kukamilisha mchakato wa mafao yako mtandaoni,” Alisema Meneja Mifumo wa NSSF, Mathayo Mihayo na kuongeza; 

“Tunataka tufikie asilimia 100 ya mambo yote kufanyika kiganjani au mtandaoni, hadithi ya mteja kusumbuliwa haitakuwapo tena, tuliona wakati mwingine unawaita wazee waje ofisi kurekebisha taarifa wakati unaweza kuwatengenezea mfumo wa kuzirekebisha kwa urahisi wakiwa kokote.”