Wazee wa CHADEMA waibuka na vilio kutetea kada yao nchi nzima

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:41 AM Oct 02 2024
Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa, Hashim Juma
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa, Hashim Juma

BARAZA la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAZECHA), limeitaka serikali kufanyia kazi kero za wazee nchini, ikiwamo kutokulipwa pensheni zao kwa wakati hali inayosababisha waishi katika hali duni na umaskini.

Pia limetaka changamoto nyingine kuwa ni kukosa huduma ya afya bure licha ya sheria  ya afya kuagiza hivyo, kukosa makazi, kukosa jukwaa la kutoa mawazo yanayogusa jamii zao, kutoshirikishwa katika mipango ya kiuchumi ya kuinua maisha yao ikiwamo mikopo na kuuawa kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Akizungumza katika hafla fupi ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa BAZECHA, Susan Lyimo, alisema ni muhimu  serikali kuzitambua na kuzitatua changamoto hizo ili kuweka mazingira mazuri kwa kundi hilo.

Lyimo alisema  serikali inapaswa kuhakikisha wazee wote hata kama hawakuajiriwa, walipwe pensheni kama ambavyo wanalipwa wenzao wa Zanzibar ili kuwaondolea changamoto za maisha na jamii kuwatumia kama tunu ya taifa.

Aliitaka pia serikali kuhakikisha mabasi ya mwendokasi yanakuwa na sehemu maalum ya kukaa wazee kama ambavyo yametengewa nafasi kwa watu wenye ulemavu.

“Wazee wamekuwa wakinyanyaswa, hawaheshimiwi, hawapewi misaada ya kimsingi na hawana mfumo wa kuwasaidia. Matokeo yake tunaona wazee hata kwenye usafiri wa umma hasa kwenye mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam, wanakosa vitu vya kukaa huku vijana wakiwa wamekalia viti bila kuwapisha,” alisema.

Kutokana na hali ngumu ya maisha  na kukosa stahiki muhimu zikiwamo huduma za afya, makazi na pensheni, alisema wazee nchini wamekuwa wakiuchukia uzee na kuukataa jambo lililozua usemi wa ‘Wazee mwisho Chalinze, mjini wote baby’.

Aidha, alisema BAZECHA imetaka  wazee hao kupigania muswada wa Sheria ya Wazee upelekwe bungeni ili ipitishwe kuwa sheria ili wapate haki zao za msingi kwa kuwa  matukio ya unyanyasaji na udhalilishaji yanaendelea kwa kundi hilo kutokana na kukosekana kwa sheria ya kuwasimamia.

Alisema tangu Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 ianzishwe, mpaka sasa haijabadilishwa na kuwa sheria ndiyo maana matukio ya unyanyasaji, udhalilishaji yanaendelea kwa sababu hakuna sheria ya kuwakingia kifua tofauti na Sera ya Watoto ambayo ilifanyiwa kazi ndani ya muda mfupi na matukio ya udhalilishaji yanadhibitiwa.

Alitoa wito kwa wazee kutoa ushauri bila kuchoka kwa watu wote hasa vijana na wenye mamalaka, kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi kwa kugombea nafasi, kupiga kura na kuhamasisha wengine kufanya hivyo.

KUTOADHIMISHWA KITAIFA

Alisema mwaka huu walipanga kufanya sherehe mkoani Mara lakini wameahirisha na kufanya kikanda kwa sababu mbalimbali ikiwamo kubadilishwa kwa tarehe ya uchaguzi wa serikali za mitaa kutoka Oktoba ilivyozoeleka hadi Novemba, mwaka huu.

Alitaja sababu ya pili ni kuahirishwa cha kwa uchaguzi ndani ya chama kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukamatwa na kuwekwa mahabusi kwa baadhi ya wagombea wa chama hicho.

“Hata wiki hii Kanda ya Pwani ilitakiwa iwe na uchaguzi lakini imeshindikana kwa sababu mwenzetu aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti yuko gerezani,” alisema.

Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa, Hashim Juma, aliwakumbusha wazee wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kupigania maslahi ya wananchi na kuacha alama.

Siku ya Wazee Duniani iliadhimishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Septemba 14, 1990 ikiwa na lengo la  kuelimisha jamii haki na stahili mbalimbali zinazohitajika kwa kundi hilo umuhimu wa uwepo wao katika jamii husika na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kuzeeka kwa Heshima’.