Yanga yaanzisha operesheni kurejea kileleni Ligi Kuu Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:05 AM Oct 02 2024
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe.
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe.

KLABU ya Yanga imesema imeanza mkakati kabambe wa kuhakikisha inakwenda kukamata nafasi ya kwanza kwenye Ligi Kuu kuanzia kesho itakapocheza dhidi ya Pamba Jiji, Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kuwa pamoja na kushinda michezo yao mitatu, lakini bado hawatokuwa na furaha hadi hapo watakapohakikisha wamekamata nafasi ya kwanza ambayo ndiyo sehemu waliyoizoea.

"Operesheni hii ni kuisaka namba moja, tutaianza rasmi Alhamisi tutakapocheza dhidi ya Pamba Jiji, niseme tu kuwa tuko katika harakati ya kuisaka nafasi ya kukaa kileleni, tumekusanya pointi tisa, tuko vizuri kidogo katika msimamo wa Ligi Kuu, ila nafasi yetu pendwa ni namba moja, tutaanza rasmi kuisaka kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji, tunaelekea kileleni na hakuna wa kutuzuia," alisema Kamwe.

Hata hivyo, Kamwe amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa jambo hilo halitokuwa rahisi kama wao watakaa majumbani,  inabidi wajazane uwanjani kwa ajili ya kuwaunga mkono viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji kwani nguvu ya pamoja inatakiwa.

"Timu ambazo hazijaanza vyema zikicheza na Yanga zinakamia sana, tuliona mchezo na KenGold, tukashuhudia dhidi ya KMC, kwa hiyo hata Pamba Jiji haitokuwa rahisi, kwa hiyo mashabiki wanatakiwa wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuungana katika mkakati wa kuelekea kwenye nafasi ya kwanza," alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William, akizungumza na gazeti hili alisema wamejiandaa kuwapa Yanga wakati mgumu katika mchezo huo.

Aidha, alikiri kuwa bado hawapo katika wakati mzuri, lakini haiwazuii kufanya vyema katika mchezo huo.

"Tunafahamu tunakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya Yanga, ni timu bora na wameanza vizuri, sisi tumeanza vibaya ingawa haimaanishi kuwa tuna timu mbaya, matokeo hayajawa mazuri upande wetu, walimu watakuwa wameona mapungufu na watayarekebisha kuelekea katika mchezo huo," alisema Ofisa Habari huyo.

Alisema katika mechi hiyo watakwenda kwa tahadhari kubwa na kuwapa heshima wapinzani wao.

Wakati Yanga ikicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiwa na pointi tisa na kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Pamba Jiji haijashinda mchezo wowote katika mechi sita ilizocheza, imetoka sare mechi nne na kupoteza miwili, inashika nafasi ya 14 kwa kukusanya pointi mbili.