Uoteshaji nywele wenye kipara wawavutia wengi Muhimbili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:01 AM Oct 02 2024
Kipara.
Picha: Mtandao
Kipara.

KITENGO cha Upasuaji Rekebishi na Upasuaji wa Urembo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinafanya upasuaji wa aina hiyo kwa wagonjwa 12 hadi 15 kwa wiki, huku mahitaji yakiendelea kuongezeka.

Huduma zinazofanywa mara kwa mara ni pamoja na upasuaji rekebishi kwa majeruhi wa ajali za viwandani, barabarani, matukio ya moto; kukiwa na wastani wa wateja (wagonjwa) sita hadi wanane kwa siku.

Hospitali hiyo ya hadhi ya juu zaidi kitaifa imesema kuwa miongoni mwa wanaohitaji huduma ya upasuaji rekebishi na idadi yao ni kubwa, ni wanaume wenye kipara.

Bingwa wa Upasuaji Rekebishi na Upasuaji Urembo MNH, Dk. Edwin Mrema, aliyasema hayo wiki iliyopita alipozungumza na Nipashe, jijini Dar es Salaam. Mwandishi wa gazeti hili alitaka kufahamu kuhusu huduma zinazotolewa katika kitengo hicho.

Alisema nchini hivi sasa ina wataalamu 10 pekee waliobobea katika upasuaji rekebishi na upasuaji wa urembo.

Alisema kitengo chao kimejikita kufanya urekebishaji wa mwonekano wa mwili, hususan wa nje kwa watu ambao wamepata ajali, wenye makovu, kasoro za mdomo, pua, masikio na kichwani.

"Kazi yetu ni kurekebisha kasoro au pale ambapo pameharibika kutokana na kasoro za duniani kama ajali au kuzaliwa. Kitengo hiki takribani miaka 18 au 20 taaluma hii inatolewa hapa ndani katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

"Huduma ambayo ni mpya ni ya kurekebisha au kufanya upandikizaji wa nywele katika kipara imeanza mwaka jana, imewavutia wengi hasa wanaume. Wengi wanaona kipara ni jambo la kawaida, ila wachache hawafurahii, wanaona ni mwonekano usiowafaa kwa wakati huo.

"Tumekwishawafanyia upasuaji wanaume sita ambao wanataka kuondokana na kipara, wanaendelea vizuri. 

"Upandikizaji nywele ni kama unavyootesha mpunga shambani, tunafanya kwa awamu hadi miezi mitatu au sita nywele zimeota," alisema bingwa huyo.

Alisema takwimu zinaonesha kipara hakichagui jinsi, huwakumba zaidi wazee kuanzia umri wa miaka 70 hadi 80 ingawa vijana walio katika umri wa kati ya miaka 20 huweza kuwa na hali hiyo pia.

"Kwa asilimia 33 wanaume watakuwa na kipara kuanzia miaka 30 na kuendelea na watahitaji upandikizaji nywele. Na wanaume wakifika miaka 50 kwa asilimia 50 watakuwa na uwezekano wa upungufu wa nywele.

"Wengi wao kwa asilimia 66 wakifikia miaka 60 watakuwa na upungufu wa nywele. Tukiangalia wengi wao duniani kulingana na asili, wanaoongoza kuwa vipara ni wazungu, Waasia, wakifuatwa na watu weusi (Waafrika) na kwa idadi ya chini sana ni Red Indians (Wahindi wekundu)," alisema bingwa huyo.

Dk. Edwin anataja sababu za baadhi kuwa na vipara ni pamoja na kurithi, kutokuwa na uwiano sawa wa homoni, msongo wa mawazo, lishe duni, mshtuko, homa na utapiamlo.

"Matumizi ya ‘contraceptives’ (uzazi wa mpango), dawa za kufifisha goita kwa watu wa kundi hili huweza kusababisha nywele kupotea. Na mwingine kuwa na kipara haina sababu na hawa siyo ‘candidate’ wazuri wa kuwafanyia upasuaji wa kuwapandikiza nywele," alisema.

*USIKOSE KUFUATILIA KESHO KATIKA GAZETI HILI MAKALA MAALUM KUHUSU KIPARA NA MATIBABU YAKE MUHIMBILI