Ahoua awaburuza Feitoto,Aziz Ki kwa 'assist' Ligi Kuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:01 AM Oct 02 2024
Jean Charles Ahoua.
Picha:Mtandao
Jean Charles Ahoua.

UKIWA ni msimu wake wa kwanza tu tangu ajiunge na klabu ya Simba, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua, ameonekana kuanza kuwa tishio kwa wachezaji wa Ligi Kuu kwa kutoa pasi za mwisho za mabao akiwa amefanya hivyo mara nne katika michezo minne aliyocheza.

Mpaka kufikia raundi ya sita, Ahoua anaonekana kuanza kuwaburuza wachezaji ambao ni wazoefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, na ambao walifanya vyema msimu uliopita kwenye 'asisti', kama Feisal Salum wa Azam, Stephane Aziz Ki wa Yanga, Clatous Chama ambaye alikuwa Simba na sasa yupo Yanga, pamoja Mohamed Hussein wa Simba.

Ahoua, raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa kutoka Stella Club d’Adjamé ya nchini humo, amecheza kwa dakika 289 katika michezo minne, akipachika mabao mawili na 'asisti' nne, ambazo alizitoa katika michezo mitatu ambayo Simba ilicheza dhidi ya Fountain Gate, Agosti 25, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba ikishinda mabao 4-0 ambapo alitoa pasi za mabao kwa Edwin Balua na Valentino Mashaka, huku mwenyewe akipachika bao moja.

Kabla ya hapo, alifanya hivyo kwa Che Fondoh Malone, Agosti 18, Simba ikicheza dhidi ya Tabora United ikishinda mabao 3-0 kwenye uwanja huo huo.

Septemba 26, Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, alitoa 'asisti' kwa Leonel Ateba, Simba ilipocheza dhidi ya Azam FC na kushinda mabao 2-0.

Ikumbukwe msimu uliopita, Aziz Ki na Kipre Junior walikuwa vinara wa 'asisti' wakiwa wamefanya hivyo mara nane.

Hata hivyo, raia huyo wa Ivory Coast anafuatiwa kwa karibu na Fei Toto, ambaye ana 'asisti' tatu alizowapa Lusajo Mwaikenda na Idd Nado katika mchezo dhidi ya KMC, wakipata ushindi wa mabao 4-0, na Nassor Saadun katika mchezo dhidi ya Coastal Union, Azam ikishinda bao 1-0.

Aziz Ki, ana 'asisti' mbili mpaka sasa, akitoa kwa Clement Mzize katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Yanga ikishinda mabao 2-0 na dhidi ya Ibrahim Hamad 'Bacca' katika mchezo dhidi ya KenGold Yanga wakishinda bao 1-0.

Wengine wenye 'asisti' mbili ni Mohamed Hussein 'Tshabalala', wa Simba, Ande Kofi wa Singida Black Stars, Salum Kihimbwa wa Fountain Gate, na Joseph Mahundi wa Kagera Sugar.