Shule ya msingi Perfect Destiny iliyopo Mkuranga, mkoani Pwani, inaendelea kuvuma kutokana na kutoa elimu bora inayochangia ongezeko kubwa la ufaulu kwa wanafunzi wake. Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Moses Masewa, taaluma inayotolewa na shule hiyo imepelekea mafanikio makubwa katika mitihani ya darasa la nne na la saba kila mwaka.
Akizungumza wakati wa hafla ya mahafali ya tano ya elimu ya awali na msingi pamoja na uzinduzi rasmi wa shule hiyo, Mwalimu Masewa alieleza kuwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba katika kipindi cha miaka minne mfululizo umefikia asilimia 100, huku wanafunzi wengi wakipata daraja A.
“Ufaulu huu wa juu umetokana na juhudi zetu kama walimu kutoa taaluma bora kwa wanafunzi, pamoja na ushirikiano mzuri kutoka kwa wazazi na walezi,” alisema Mwalimu Masewa. Hata hivyo, alitaja changamoto ya baadhi ya wazazi kuchelewesha malipo ya ada, jambo ambalo limekuwa kikwazo katika utekelezaji wa mipango ya shule.
Alisema katika kipindi kifupi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020, Shule ya Perfect Destiny imepiga hatua kubwa, ikiwemo kuanzisha Sekondari yenye madarasa ya kidato cha kwanza na cha pili. Hii ni hatua nyingine inayodhihirisha nia ya shule hiyo kuboresha zaidi sekta ya elimu katika wilaya ya Mkuranga na kanda nzima.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Diwani wa Kata ya Vikindu, Mohamed Mahundu, aliwasihi wazazi na walezi kuendelea kuunga mkono jitihada za shule hiyo kwa kuwapeleka watoto wao hapo. "Shule hii imeendelea kuitangaza Mkuranga kutokana na matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa na kikanda. Hivyo ni muhimu wazazi kuendelea kuleta watoto wao ili wapate elimu bora," alisema Mahundu.
Aidha, mkurugenzi mtendaji wa shule hiyo, Abraham Shafuri, aliwahakikishia wazazi kuwa shule hiyo imesajiliwa rasmi na ina vibali vyote vya serikali, huku akielezea mipango ya shule kuwa na maabara za kisasa za sayansi pamoja na kuanzisha madarasa ya kompyuta ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza sayansi na teknolojia kwa ufanisi zaidi.
Alisema Shule ya Perfect Destiny imejipambanua sio tu kwa kutoa elimu bora, bali pia kwa kuhakikisha wanafunzi wanalelewa katika maadili mema na mazingira salama. Hii imepelekea kuwa kivutio kwa wazazi wengi wanaotaka watoto wao kujiunga na shule hiyo.
Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Shafuri alibainisha kuwa shule hiyo imejipanga kujenga nyumba za walimu ili kuboresha maisha yao na kuhakikisha wanatoa elimu kwa moyo mmoja. Aidha, aliomba serikali kusaidia katika mipango ya kuwawezesha wanafunzi kupata lishe bora kwa kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki na ng'ombe katika shule hiyo.
Shule ya Perfect Destiny inaendelea kuwa mfano wa kuigwa na shule nyingine kwa kutoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu na maendeleo ya kijamii katika mkoa wa Pwani. Wazazi na walezi sasa wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya elimu ya watoto wao, pamoja na kushiriki katika uchaguzi wa vijiji na serikali za mitaa kwa ajili ya kujenga jamii yenye amani na maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED