Hukumu kesi ya ‘Binti wa Yombo’ yawaibua wadau

By Augusta Njoji ,, Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:20 AM Oct 02 2024
Hukumu kesi ya ‘Binti wa Yombo’ yawaibua wadau
Picha: Mtandao
Hukumu kesi ya ‘Binti wa Yombo’ yawaibua wadau

HUKUMU ya kifungo cha maisha gerezani katika kesi ya kubakwa na kulawitiwa binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, imeibua furaha kwa wadau wa sheria na haki za binadamu.

Wamesema wamefurahishwa namna kesi hiyo iliyovuta hisia kitaifa, ilivyoendeshwa kwa haraka na kutoa hukumu wanayodai inatenda haki.

Hata hivyo, wameshauri shauri la afande anayedaiwa kuwatuma vijana hao nalo liendeshwe haraka ili kukamilisha utoaji haki dhidi ya tukio hilo.

Akizungumza jana na Nipashe kwa simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga alisema hukumu ya kifungo cha maisha gerezani na faini waliyopigwa na mahakama katika kesi hiyo, imetolewa kwa wakati na kwa kufuata Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, inayoelekeza adhabu ya namna hiyo kwa mtu ambaye amefanya kosa la kubaka kwa kundi.

"Tunaona haki imetendeka, wito wetu ni kwamba kesi zingine ziwe zinachukua muda mfupi kama hii, hasa za jinai, kuna kesi zinachukua muda mrefu, miezi minane hadi mwaka," alisema.

Mwongozo wa Utendaji wa Mahakama unaelekeza kesi ndogo zishughulikiwe na mahakama ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita na kesi kubwa zisikilizwe ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Hata hivyo, ripoti ya ukaguzi maalum wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka 2020/21 kuhusu haki jinai nchini, inabainisha kuwapo ukiukwaji wa mwongozo huu katika utendaji wa mahakama, hali ambayo anaitaja inasababisha kuwapo msongamano mkubwa wa mahabusu katika magereza nchini.

Katika mazungumzo yake na Nipashe, Mkurugenzi Dk. Anna pia alisema wanahitaji kuona watu wote waliohusika katika tukio la Binti wa Yombo kubakwa na kulawitiwa, wanafikishwa mahakamani, akiwamo afande anayedaiwa alituma vijana hao kufanya ukatili huo.

"Kesi yake isikilizwe na haki ikamilike kutendeka," alitamka kwa hisia kali Mkurugenzi huyo wa LHRC.

WAZIRI GWAJIMA

Kupitia mtandao wake wa X, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, juzi alirusha taarifa ya hukumu hiyo na kuibua maoni ya wasomaji.

Mmoja wa wasomaji hao aliandika, "Tunashukuru kwa wote tuliochukizwa na lile tukio, walau mmetufuta machozi. Watanzania hii ndiyo haki tunayoililia. Sasa swali vipi kuhusu afande?"

Kutokana na swali hilo, Waziri Gwajima alisema, "Ninajaribu kuwaza kama wewe, kuwa hawa waliosema wametumwa, wao si ndiyo wangethibitisha huko mahakamani ambako mimi na wewe hatukuwapo. Kumbuka mimi na wewe hatuna mamlaka ya kuingilia shauri la mahakamani…

"Ila hao waliohukumiwa ndiyo walikuwa na fursa ya kusema tulitumwa na ushahidi huu hapa na mahakama iamue. Hivyo, ninaomba niishie hapa kuheshimu uamuzi wa mahakama tulivyosikia na ambaye hajaridhika, ninadhani huwa kuna fursa ya rufani. Asante sana," alisema Waziri Gwajima.

MWABUKUSI

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi alisema hukumu hiyo ni salamu tosha kwa wahalifu kuwa uhalifu haulipi.

"Nimefarijika sana kwa hukumu hii na kwa usikilizwaji wa kesi hii kwa wakati, lakini wakati mwingine mahakama isizuie wadau muhimu kuhusika katika usikilizaji kesi za mazingira kama haya," alisema Mwabukusi.

MARY CHATANDA

Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) pia imepongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa kile inachodai "kutenda haki kwenye kesi hiyo".

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mary Chatanda alisema, "UWT inatoa pongezi kwa mahakama kwa kusimamia sheria na haki kwa kuhakikisha waliofanya kitendo hiki cha kinyama wanapata adhabu stahiki na ni ushindi mkubwa wa mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia."

Alisema UWT inatoa wito kwa watanzania kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kukithiri katika jamii, yakiwamo matukio mawili yaliyotokea hivi karibuni mkoani Tanga, ili kulinda haki na utu wa binadamu.

Juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma iliwahukumu kifungo cha maisha gerezani pamoja kulipa faini ya Sh. milioni moja kila mmoja vijana wanne waliokutwa na hatia ya kumbaka na kumlawiti binti huyo.  

Waliohukumiwa na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo, Zabibu Mpangule ni aliyekuwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, aliyekuwa Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema, maarufu Kindamba.