TRA yaandika rekodi mpya makusanyo

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 09:29 AM Oct 02 2024
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda
Picha:Mtandao
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imevunja rekodi yake ya makusanyo, ikikusanya zaidi ya Sh. trilioni 3.1 kwa mara ya kwanza ndani ya mwezi mmoja (Septemba mwaka huu).

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati anatoa taarifa ya utekelezaji na usimamizi wa mapato ya kipindi cha robo mwaka (Julai hadi Septemba) mwaka huu.

Alisema kiwango cha makusanyo hayo hakijawahi kufikiwa na mamlaka hiyo tangu kuasisiwa kwake.

Alisema kuwa tangu akabidhiwe majukumu ya kuongoza mamlaka hiyo, kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu, waliweka lengo la kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh. trilioni 7.4, lakini wamevuka lengo kwa kupata zaidi ya Sh. trilioni 7.7.

Mwenda alisema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri wa sheria za kodi, kuzuia mianya ya rushwa, kuweka mazingira rafiki ya ulipaji kodi pamoja na kusikiliza na kutatua vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara.

"Tumeandika historia mpya tangu mamlaka yetu ianze kazi. Kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka huu pekee tumefanikiwa kukusanya kodi kiasi cha zaidi ya Sh. trilioni 3.1.

"Ni jambo la kujivunia na kupongeza wafanyakazi na walipakodi wote nchini, mafanikio haya yanatokana na kusikiliza na kutatua vikwazo vya wafanyabiashara kwa wakati," alisema Mwenda.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na maagizo aliyoyatoa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu TRA katika kutimiza majukumu yake, akihitaji uadilifu, usawa, kusimamia sera nzuri za uwekezaji na kujenga uhusiano mzuri na walipakodi ili kuhakikisha kodi stahiki inakusanywa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo.

Alifafanua kuwa TRA waliweka lengo ambapo kwa mwezi Julai walifanikiwa kukusanya asilimia 105 ya mapato, Agosti alikuwa asilimia 104 na Septemba 105.

Alisema kuwa TRA wataendelea kutekeleza maagizo ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwasikiliza wafanyabiashara, kuwafuata walipo na kuweka mazingira sawa ya kufanya biashara kila mmoja kulipa kodi stahiki bila upendeleo.

Alisema kuwa ili kufanikisha hayo, Watanzania wanapaswa kudai na kutoa risiti wakati wa ununuzi na uuzaji.

Aliongeza kuwa TRA wamekusudia kuweka nguvu na kuimarisha kitengo cha ukaguzi na uchunguzi ili kudhibiti mianya ya upotevu mapato, yakiwamo maeneo ya forodha.

Kamishna wa Forodha, Juma Hassan, alisema wamepanga kuboresha usimamizi wa mifumo ya kuhudumia wateja wao, ambayo itaanza kutumika kuanzia Januari mwaka 2025.

Alisema mifumo hiyo itafanya kazi hata kwa mteja akiwa ofisini kwake na itaokoa muda na gharama za kufuata huduma hiyo katika ofisi za forodha, alidai mifumo itasomana.

Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa, Michael Muhoja alisema asilimia 43 ya mapato ya TRA inatokana na kodi za wafanyabiashara wakubwa.

Alisema katika kutekeleza majukumu yao wamegawana majukumu; kuna watumishi wanaohudumia masuala ya madini, viwanda na taasisi nyingine.

Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi aliwataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu zao, kutii sheria za ulipaji kodi na kuzingatia nyakati za kulipa kodi ili kuepuka faini.