Boni Yai kupigiwa kura akiwa gerezani, uchaguzi uwenyekiti Kanda ya Pwani

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 07:22 PM Oct 02 2024
Aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai, akiwa mahakamani.
Picha: Mtandao
Aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai, akiwa mahakamani.

MKURUGENZI wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, amethibitisha kwamba aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai, atapigiwa kura kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Pwani licha ya kuwa bado yupo gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.

Boniface Jacob na Gervas Lyenda, waliteuliwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Septemba 17 mwaka huu, kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Pwani. 

Hata hivyo baada ya mchakato wa uchaguzi kuanza, zikiwamo kampeni, Septemba 18, mwaka huu, Boniface alikamatwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alithibitisha na kukiri kumshikilia Boniface akidai ni kwa makosa ya kijinai anayotuhumiwa.

Boni Yai. yuko gereza la Segerea kutokana na dhamana yake kusubiri hatma ya kupata, ambayo imepangwa kutolewa Oktoba 7, mwaka 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Baada ya uamuzi wa mahakama kuhusu dhamana ya Boni Yai, uongozi wa Chadema Kanda ya Pwani, umeamua kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa ukitarajiwa kufanyika Kibaha mkoani Pwani.

Hata hivyo, Oktoba 5, 2024, Kanda ya Pwani ya Chadema yenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, itafanya uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa kanda hiyo.