Bei za mafuta zashuka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:59 PM Nov 06 2024
Bei za mafuta zashuka
Picha: Mtandao
Bei za mafuta zashuka

Bei za reja reja za mafuta kwa mwezi Novemba 2024 zimeendelea kushuka ambapo bei ya petroli kwa Dar es Salaam na Tanga imeshuka kwa asilimia 2.26 ambayo ni sawa na sh.68 kwa lita, huku Mtwara ikiwa imepungua kwa asilimia 2.16, ikilinganishwa na bei za mafuta za mwezi Oktoba 2024.

Aidha, bei ya dizeli pia imepungua kwa asimia 0.07  kwa Dar es Salaam, asilimia 0.17 kwa Tanga na asilimia 0.11 kwa Mtwara.
 
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo Novemba 6, 2024, imeeleza kuwa ahueni hiyo kwa bei za mwezi huu, inatokakana na kushuka kwa gharama za kuagiza mafuta ya petroli kwa wastani wa asilimia 3.91 na kupungua kwa
gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa wastani wa asilimia 1.75.
 
Kutokana na punguzo hilo, petroli mkoa wa Dar es Salaam itauzwa kwa sh.2,943 kwa lita, Tanga sh.2,948 na Mtwara sh. 3,015. Kwa upande wa dizeli, bei za rejareja kwa mwezi Novemba 2024, Dar es Salaam ni sh.2,844 kwa lita, Tanga sh.2,855 na Mtwara sh. 2,916.  Mafuta ya taa yatauzwa sh.2,943 Dar es Salaam, sh. 2,989, Tanga na sh. 3,016 Mtwara.