Awataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa kiwanda cha nondo, saruji Njombe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:58 AM Oct 21 2024
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian.
Picha:Mtandao
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian.

WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, wilayani Njombe, wametakiwa kutumia fursa ya kuwapo kiwanda cha kuzalisha nondo, saruji na kuunda magari kinachojengwa kijiji cha Ikelu, kwa kujenga nyumba na hoteli za kisasa, ili wanufaike kiuchumi.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na kisiasa mkoani Njombe, Oraph Mhema wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Makambako. 

Alisema kutokana na ujenzi wa kiwanda hicho, wafanyabiashara wanatakiwa kuwekeza katika ujenzi wa hoteli za kisasa, kwa kuwa kiwanda hicho kitasababisha mwingiliano wa watu ambao ni lazima watahitaji huduma ya chakula na malazi. 

Mhema alisema kuwa mbali na fursa hiyo kwa wafanyabiashara, serikali pia inatakiwa kujenga chuo cha ufundi mjini Makambako, ili kuzalisha wataalamu ambao watafanya kazi katika kiwanda hicho badala ya kuajiri watu kutoka nje ya mkoa huo.

"Makambako kwa sasa ninaiona mbali sana, serikali sasa itumie fursa hii kuleta vyuo vya ufundi, ili tusibaki nyuma kwenye mpango huu wa viwanda kwa sababu kama hatuna taaluma yoyote, tutabaki nyuma na watakuja wageni watachukua fursa za kwetu," alisema Mhema. 

Baadhi ya wananchi mjini Makambako, akiwamo Zawadi Chusi, walisema kujengwa kiwanda hicho kutakuza uchumi wao kutokana na kuongezeka mwingiliano wa watu pamoja na vijana wengi kupata ajira.

 "Kwa ujenzi wa kiwanda hiki ni faida kwetu sisi Makambako, kwa sababu sisi wanawake tupo tunazunguka kuuza matunda, uji. Kwahiyo, ujio wa hiki kiwanda utatusaidia sana kuinua uchumi wetu na kutusaidia kupeleka watoto shuleni," alisema Zawadi. 

Oktoba 10, mwaka huu, Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, alitembelea eneo ambalo kiwanda cha kuzalinda nondo, saruji na kuunda magari kinachojengwa katika kijiji cha Ikelu na kampuni ya Fujian Hexingwang Industry.  

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 500.