INAPOZUNGUMZIWA kanuni zinazomsaidia mtu kuwa na uchumi imara katika maisha yake, si wote wanaozifahamu.
Ili mtu aweze kufanikiwa kiuchumi, iwe binafsi au kwa biashara, anatakiwa kuzingatia kanuni zifuatazo:
Hizo zinajumuisha kubadilisha mtazamo na mawazo yanayohusiana na dhana mafanikio, kukiwapo maono au ndoto chanya, zikiguswa na kufanya kazi kwa bidii, ubora na uaminifu.
Vilevile, kuna maoni yanayogusa maeneo: Nidhamu ya fedha na kubana matumizi; kuwa na utamaduni wa kuweka akiba; na kujiepushe na madeni.
Pia, kukaongezwa dhana ya kutunza afya ambayo ni mtaji mkubwa sana katika kufanikiwa afya na uhai, analitaja mshauri huyo kuwa suala la baraka kuu kiimani, pasipo kusahauliwa mahitaji ya kibinadamu.
Hapo yanaorodhesha mazoezi ya mwili; kunywa na kula, pia kupata mwanga wa jua, kuvuta hewa safi, pia kupumzika.
Mchungaji Lucas Mwimo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloitwa Tanzania Prisoners Hope Foundation (TPHP), ametamka hayo katika mazungumzo na wanawake waliomaliza vifungo magerezani.
Mchungaji Mwimo, akawaasa kuepuka tamaa, hasa wanapoona uchumi wako umeanguka au hauendi vizuri.
“Hofu ni mlango ambao adui au shetani anautumia ili kumtesa mwanadamu, hofu huondoa tumaini na nguvu ya imani, kwa hiyo jitahidi kukataa hofu na kukata tamaa,” anasema.
KANUNI YA KWANZA
Inatajwa kuwa ili mtu abadilishe mitazamo kwa mtazamo wake, kuhusu dhana ya mafanikio.
Mitazamo inarejewa kuwa picha ya ndani ya mtu kuhusu jambo fulani, kutokana na mawazo na maamuzi yanayofanya kila siku yakitafsiri kushinda au kushindwa kimaisha.
Mwimo anaeleza: “Aina ya mawazo na mtazamo inaamua hatima ya maisha utakayoishi, ama maisha ya juu, kawaida au umaskini.
“Jitahidi kukataa mawazo ya kinyonge na mtazamo mbaya wa kushindwa. Ukitaka kufanikiwa na kuwa na uchumi bora, shikilia mtazamo wa ushindi, utele na utajiri katika mawazo yako.“
KANUNI YA PILI
Maono anayataja kuwa picha ya ndani kimaisha, mtu anataka ama kuishi nayo au walau kuyafikia, ngazi ya nafsi au maisha mtu anataka kuyafikia baadaye.
Anataja hatua kuu ya kwanza, ni kujiwekea maono binafsi, akiwa na ufafanuzi kwamba asiye na maono, daima anakosa mafanikio, kila mtu aliyefanikiwa alianza kwa maono.
“Jitahidi uwe na picha ya maisha yako, jitahidi upajue unapokwenda na hapo yalipo maisha na mafanikio yako, moja ya sifa za watu wakuu waliofanya makubwa duniani na kuacha alama ni maisha ya maono,” anasema.
FAIDA YA MAONO
Kuna maono yanayompa mtu uwajibikaji na kuukomboa wakati, yanampa nidhamu.
Mwimo anasema kwamba kila mwenye maono, ni lazima kujiwekea nidhamu ya nini cha kufanya na nini cha kutofanya ili kufikia ndoto yake.
Pia, anatetea maono kwamba, huamua mtu anakopaswa kupafikia, akinena kanuni ni mtu ana nafasi ya kufikia anakopabashiri, yakimpa lengo na kujiandaa vizuri kuyatekeleza.
BIDII, UBORA, UAMINIFU
Mwimo anasema, fedha na utajiri hupatikana kupitia kufanya kazi na shughuli halali za kiuchumi.
“Ili ufanikiwe, fanya kazi au biashara na shughuli za kiuchumi kwa bidii na kwa uaminifu. Hakuna aliyefanikiwa katika maisha bila ya kufanya kazi kwa bidii...” anatamka Mchungaji Mwimo.
“Tusifanye kazi bora liende, bali kwa ubora. Kitakachokupa wateja na kibali ni ubora wa bidhaa unazozalisha, pia kitakachokupa ‘promosheni’ kazini, ni ubora wa kazi unazozifanya!” anasema
KANUNI BORA KIBIASHARA
Mwimo anataja biashara ni kazi za kuinua uchumi, hasa inapofanywa kwa kufuata kanuni za kiuchumi na biashara.
Baadhi ya kanuni za kufanikisha biashara yako ni kama: Kufanya utafiti wa kutosha na kujiridhisha biashara hiyo inaleta faida.
Pia, Mwimo akaeleza kuwapo soko au wateja wa kudumu wa kununua bidhaa au huduma, huku akitaja biashara ni kitu muhimu, hasa inapokuwa katika sehemu nzuri.
Kwa biashara za rejareja, kunatajwa panafaa mahali penye watu wengi wanakopita, wakichagua fursa au masoko na mauzo ya jumla.
Anataja kanuni nyingine ni kuwapo muuzaji makini, mchangamfu na anayesikiliza na kuwajali wateja, ikiendana na analolitaja kuwa suala la ‘Mteja ni Mfalme.’
Hapo Mchungaji Mwimo ana ufafanuzi wake kuwa:“Hii itasaidia kujenga uhusiano mzuri kati yako na wateja wako.
“Ni lazima uwashawishi, kwanini waje kununua kwako na sio kwa wengine, pia usafi wa mazingira ya biashara na usafi wa muuzaji.”
Pia, wanasisitizwa wahusika kutouza vitu viliyokwisha muda wake (vyakula), mbadala wake kuwekewa vivutio mbalimbali, kama vile kupunguza bei kwa baadhi ya vitu.
Hiyo anaitaja inaendana na kuwapo matangazo ya utambulisho wa biashara kuwavutia wateja, pia ukopeshaji kwa wateja waaminifu.
Vilevile inaendana na biashara hiyo ikifunguliwa kwa wakati sahihi, hakuna kauli za hasira kwa wateja na ina hamasa
“Kwa mfano. kama wateja wanaulizia bidhaa hiyo hiyo na wewe hunayo, nenda ukaitafute,” anasema Mwimo.
Eneo lingine linatajwa, ni kuweka aina nyingi za bidhaa kumuwezesha mnunuzi anunue vitu mahali, pamoja, huku wenye biashara kiserikali na sekta nyinginezo zinazomhusu, akiwajibika kulipa kodi.
Hapo inaendana na kuwapo daftari lake la kutunza hesabu inayomhusu.
KANUNI YA NNE- KUWA NA NIDHAMU YA FEDHA NA KUBANA MATUMIZI (FINANCIAL DISPLINE)
Mafanikio ya kiuchumi/biashara yanahitaji nidhamu ya fedha na matumizi, kinachofanya watu wengi washindwe kufikia ndoto za mafanikio ya uchumi na maisha yao ni tatizo la matumizi mabaya ya fedha yasiyo na nidhamu.
Anasema, sababu kubwa ya watu kutoweka akiba ni kutodhibiti matumizi na ukishaweza kujizuia kwenye matumizi, tegemea utajiri.
“Matumizi ndiyo yanayoamua hatima ya utajiri au umaskini, umaskini ni hali ya matumizi yako kuwa makubwa kuliko kipato chako, jifunze kuweka vipaumbele juu ya mahitaji muhimu utakayo fanya kwa pesa iliyopo mkononi mwako na usijaribu kutaka kutekeleza kila hitaji,” anasema
Anasema, mahitaji ni mengi hutaweza kuyamaliza, michango ni mingi hutaweza kumchangia kila mtu, kukiwapo maisha ya uhalisia na kuepuka matumizi ya fedha.
Hiyo inatajwa, ili kuwaridhisha wanadamu pamoja na ndugu zako na moja ya kitu kitakachokusaidia kuwa na matumizi mazuri ni kuandaa bajeti na kuiheshimu.
MAANA YA BAJETI
Bajeti maana yake ni kuoanisha mapato na matumizi, kupanga na kutawala matumizi, kupanga bajeti ni kwa muhimu kama vile ilivyo muhimu kufanya kazi, bajeti inayofanikiwa ni lazima izingatie mambo yafuatayo:
Bajeti ni lazima itokane na mapato na sio mategemeo, lazima iwe ya kweli na ya utaratibu, fedha ni lazima zipangwe kulingana na hitaji la kweli, mume na mke ni budi wafanye pamoja kufanikisha bajeti yao.
“Bajeti inaweza kuwa ya wiki au ya mwezi kutegemeana na vyanzo vya mapato, bajeti yenye mafanikio inahitaji utaratibu wa kutunza mahesabu.
“Hiyo ni kama vile, kuwa na kitabu cha bajeti kuandika manunuzi yote, au bahasha zinazofichwa kwa usalama zenye fedha zote zilizopangwa...,” anasema
Pia, anataja, penye mapato yasiyoendana na uhalisia wa mahitaji, inapaswa kufanyiwa marekebisho ama kwa kupata mapato zaidi au kuyapunguza.
KUWEKA AKIBA
Anasema lengo la kuweka akiba, ni kupata fedha za dharura, ili kujiepusha na mikopo isiyokuwa ya lazima na kupata fedha ya mtaji kwa ajili ya uwekezaji.
Pia, anafafanua kuwa mtu anatakiwa kuweka akiba kwa kila fedha unayoipata na kuiweka kwenye akaunti kwenye benki, kibubu, au simu, kila fedha inayoingia mikononi mwako ina mkate na mbegu (Akiba).
Pia, kunatajwa kuwapo watu waliofanikiwa sana katika maisha na wamejitahidi kujinyima, hata kujijengea mazoea ya kuweka akiba kwa awamu.
Mwimo anaendelea kuwaasa: “Tofauti ya masikini na tajiri ni kwamba maskini akipata pesa anakula kwanza kisha anawekeza kama itakuwa imebakia.
“Tajiri akipata pesa, anawekeza kwanza, kisha anakula inayobaki. Hakuna tajiri asiyeweka akiba. Mweka akiba yupo kwenye njia ya utajiri,” anafafanua katika mada yake.
Hapo anawaasa kinamama hao, kujenga tabia ya kutenga akiba kabla ya matumizi, mathalan asimilia 10 ya mapato ni hali inayomkingia mtu adha ya madeni yasiyo ya lazima, kwani asiyeweka akiba hawezi kukwepa madeni.
Hapo anawapa kanuni kwamba, “adui mkubwa wa kuweka akiba ni kuahirisha” na wito wake ni kwao kuanza hilo mara moja.
KANUNI YA SITA
Hatua hiyo, anawasisitizia kuepuka madeni na mikopo pale inapobidi au hakuna ulazima wake, isipokuwa katika ulazima au dharura. Mtazamo ni kwamba ‘madeni sio dhambi, ila ni mzigo na utumwa unaotunyima pumziko.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED