Tetesi 11 za usajili zinazotikisa Bongo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:59 PM Jun 03 2024
news
Picha: Maktaba
Nyota wa Simba, Mzambia, Clatous Chama.

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara imemalizika, tayari baadhi ya timu zimeshaanza mchakato wa kusaka wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Na hii haipo hapa nchini tu, hata Ulaya na kabla ya hapo, klabu zipo kwenye mikakati ya kusajili wachezaji ili kuongezea nguvu vikosi vyao.

Hapa nchini tetesi mbalimbali zimeanza kusikika kwa baadhi ya wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine. Pia viongozi wa timu baadhi yao, akiwamo Rais wa Yanga, Hersi Said, walisafiri nje ya nchi, ambapo pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha wanapata nyota wazuri kwa ajili ya msimu mpya.

Katika makala hii tutaangalia tetesi za usajili zinazovuma kwa sasa na majina ya wachezaji wanaotajwa kuhamia kwenye klabu mpya.

 1. Mayele kutua Simba SC

 Tetesi hizi zilianza tangu katikati ya msimu wa ligi kipindi cha dirisha dogo, lakini kuelekea mwishoni mwa ligi, straika huyo wa zamani wa Yanga, ambaye kwa sasa anaichezea Pyramids ya Misri, anatajwa kutaka kuhamia Simba.

Zipo habari zinasema nyumba aliyokuwa akiishi straika, Jean Baleke ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kama ilivyo Fiston Mayele, imeandaliwa kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye uwezo wa kufumania nyavu. 

2. Kinzumbi atajwa Yanga 

Winga machachari wa TP Mazembe, Phillipe Kinzumbi, anatajwa atatua kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kuanza kazi kuelekea msimu mpya.

Tetesi zinasema safari ya Hersi huko DRC na viongozi wa TP Mazembe kuja nchini, pamoja na mambo mengine ilikuwa ni harakati za mabadilishano ya wachezaji kwa timu zote mbili.

Inasemekana Yanga imekubali kumwachia, Kennedy Musonda, ambaye alitakiwa sana na TP Mazembe wakati alipokuwa Power Dynamos, lakini ikamkosa na kutimkia Yanga, lakini kwa sasa itampata kwa makubaliano rasmi.

Yanga inadaiwa kutoa mchezaji huyo pamoja na fedha kidogo kwa ajili ya kumpata Kinzumbi. 

3. Lyanga kutimkia Simba 

Inaelezwa Ayoub Lyanga amegomea mkataba mpya na Azam FC, chanzo kikisema anataka kujiunga na Simba ambako pamoja na dau la usajili, lakini wamemwekea mshahara wa Sh. milioni 10 kwa mwezi.

Mkataba wa mchezaji huyo na Azam utatamatika mwishoni mwa msimu. 

4. Chama mguu Simba, mguu Yanga 

Nyota wa Simba, Mzambia, Clatous Chama, inatajwa huenda akajiunga na Yanga msimu ujao kama Simba hawatamwongeza dau analohitaji.

Tetesi zinasema, mchezaji huyo anahitaji kulipwa Sh. milioni 700 ili asaini mkataba mpya, lakini klabu imegoma na imemwekea ofa ndogo ambayo inaamini  inamfaa kutokana na umri pamoja na uwezo wake wa sasa.

Chanzo kinasema klabu imemwambia kama anaona ndogo basi anaweza kwenda popote anapoona anaweza kuipata pesa hiyo, huku taarifa zinasema hiyo ni habari nzuri kwa Yanga ambayo inamwania kwa misimu kadhaa.

Mpaka sasa kuna hamsini kwa hamsini, anaweza kubaki Simba, au kwenda Yanga. 

5. Mkude anabakia Yanga 

Kuna mazungumzo ambayo yamefikia pazuri kati ya menejimenti ya kiungo mkabaji, Jonas Mkude na uongozi wa Yanga kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya wa kusalia kwenye klabu hiyo.

Mkude ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga akitokea Simba, ameonekana kuwavutia mabosi wa klabu hiyo mpya, hasa katika mechi za mwisho za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

6. Kibwana atakiwa Simba 

Beki wa kulia wa Yanga ambaye ana uwezo wa kucheza upande wa kushoto, Kibwana Shomari, anaonekana kuwindwa na Simba kwa ajili ya kwenda kumsaidia, Shomari Kapombe.

Kibwana ambaye anamaliza mkataba wake mwishoni mwa simu huu, inasemekana waajiri wake wa sasa hawajafikia dau analohitaji, hivyo inaweza kurahisisha mchakato wake wa kutua kwa Wekundu wa Msimbazi. 

8. Kagoma abadili gia angani 

Kiungo mkabaji aliye katika kiwango cha juu msimu huu, Yusuph Kagoma wa Singida Fountain Gate, awali alitajwa kuhitajika Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

Hata hivyo, Simba iliingia kati dili na mwenyewe akabadilika, akitaka kwenda kucheza Msimbani kwa kile kilichoelezwa ni wepesi wa kupata namba. 

9. Lawi wa kwanza Simba 

Tetesi zinasema beki wa kati ya Coastal Union, Lameck Lawi, ndiyo wa kwanza kusajiliwa na Simba msimu huu.

Habari zinasema alisaini wiki mbili zilizopita kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili. 

10. Matampi awakuna Simba 

Uwezo wa golikipa Mkongomani, Ley Matampi, umeonekana 'kuwakuna' viongozi wa Simba, ambao sasa wameonyesha nia ya kutaka kumsajili.

Kipa huyo aliyesajiliwa na Coastal Union na kusimama langoni mechi 16 bila kuruhusu bao akimpiku kipa wa Yanga, Djigui Diarra, anaonekana anaweza kuisaidia timu hiyo ambayo imeonekana kuruhusu mabao mengi msimu huu. 

11.Mwamnyeto lulu Simba 

Viongozi wa Simba wanatajwa kumhitaji beki wa kati ya Yanga, Bakari Mwamnyeto ili kuongeza nguvu ya ulinzi pale kati. Beki huyo ambaye Simba ilimkosa miaka kadhaa iliyopita alipokuwa Coastal Union na kutua Yanga, bado yupo vichwani kwa mabosi, wakiamini atawasaidia, huku mkataba wake wa timu yake ya sasa ukitamatika.

Habari zinasema Simba imeweka dau kubwa mezani, kuliko la Yanga ambalo wamempa mchezaji wao.