HADI sasa katika azma na dhamira ya serikali imedhamiria kuwezesha na kuinua wanawake kiuchumi, kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwapa mitaji ya fedha na kuwatafutia vitendea kazi kwa wafadhili.
Ipo mifano mingi, miongoni mwake ni msaada wa hivi karibuni wa cherehani 425 na mashine 250 za kutotolea vifaranga vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 79 vilivyotolewa na serikali ya China.
Msaada huo ulikabidhiwa kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima na Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian.
"Cherehanii hizi na mashine ya kutotolea vifaranga, tutashirikiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM Taifa (UWT), mama yetu Mary Chatanda kuwatafuta wanawake tutakaowaibua hasa wenye uhitaji na kuwapelekea," anasema Dk. Dorothy.
Anafafanua kuwa wajasiriamali 675 watanufaika na msaada huo, huku cherehani 300 na mashine zote za kutotolea vifaranga vitapelekwa katika vikundi vinaratibiwa na wizara yake, lakini cherehani 125 vitapelekwa kwa vikundi vilivyo chini ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).
Dk. Dorothy anasema vyerehani na mashine hizo, zinagusa ahadi mbalimbali za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwezesha wanawake kiuchumi, na kwamba yeye (Rais) ni kinara wa kuwezesha wanawake.
"Wanajitokeza marafiki wa Tanzania walioilewa falsafa ya Rais Samia. Sisi wizarani tunapokea wageni wengi wanauliza kuna nini kwa wanawake, tunawapa takwimu na kuwaeleza programu ya kuwezesha wanawake kiuchumi ambayo kinara wake ni Rais Samia," anasema.
Anasema hadi sasa serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 inayotoa kipaumbele kuwezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuondoa ukatili wa kijinsia.
"Serikali inatambua umuhimu wa wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi, hivyo msaada huu wa ndugu zetu wa China, utakuwa chachu kwenye programu ya uwezeshaji wanawake kiuchumi," anasema.
Aidha, anasema hadi sasa, kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, tayari Sh.bilioni 743.7 zimeshatolewa na kunufaisha Watanzania 6,064,957, wakiwemo wanawake 3,556,359 sawa na
asilimia 54, wanaume wakiwa ni 3,288,186 sawa na asilimia 46.
NENO TOKA UWT
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda anasema kampeni za uchaguzi zinahitaji fedha na kuongeza kuwa wanawake wengi hawana vipato vya kutosha, na kwamba hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwezesha wanawake kiuchumi zitawafanya wajitokeze kwa wingi.
"Umaskini wa kipato unawafanya wanawake wengi kubaki nyuma, lakini ninaamini wakiwezeshwa kiuchumi, wanaweza kupambana na wanaume hadi tukafikia asilimia 50 kwa 50 tunayoitafuta," amesema Mary.
Anasema UWT imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kutaka kuwainua wanawake kiuchumi ikiwamo msaada wa vifaa vya uzaalishaji mali na pia kutoa elimu ya kuwawezesha kupata mikopo.
"Tunawahamasisha kujiunga katika vikundi, ili wapate mikopo ikiwamo inayotolewa na halmashauri, lakini kuna msaada wa vitu ambalimbali tunaopata ukiwamo huu vyerehani kutoka China," anasema.
Mary anasema, kwa sasa umoja huo unajiandaa kuzunguka nchi nzima kwenda kushirikiana na maofisa maendeleo ya jamii kwa lengo la kutoa elimu kwa wanawake jinsi ya kutumia mikopo.
"Kuna mikopo inayotolewa na halmashauri zetu, tunataka tuwafundishe jinsi ya kuipata na kuitumia kwa usahihi, sio kwenda kununua vitenge, kwa sababu ehaviwezi kurejesha mkopo," anasema.
Anasema, wanawake wakiimarika kiuchumi, wana uwezo wa kuwania uongozi na kushinda bila kuingia katika mtego wa rushwa ya ngono ambayo wamekuwa wakikumbana nao na kuamua kukaa pembeni.
"Bila nguvu kiuchumi, ushiriki wa wanawake katika siasa unaweza kuwa kitendawili na kuongeza kuwa ni muhimu kutekeleza Azimio la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), linalotaka ushiriki wa wanawake na wanaume katika fursa za uongozi kuwa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030," anasema.
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian anasema, nchi yake imekuwa ukitoa misaada mbalimbali ya kuwanufaisha wanawake wa Tanzania, ili kuimarisha ustawi wa wananchi, na kwamba waliotoa utawasaidia walengwa kuongeza kipato.
"Kwa miaka miwili ambao nimefanya kazi Tanzania, nimejionea Rais Samia akitilia mkazo masuala yanayohusu wanawake na kushuhudia baadhi ya wanawake wenye uwezo mkubwa," anasema Chen.
Anasema, China na Tanzania zina ushirikiano mzuri, na kufafanua kuwa anafurahi kuona ushirikiano huo unazaa matunda, na kwamba China ilishwahi kutoa mbegu za soya kwa wakulima wa mkoa wa Ruvuma.
Vilevile, tumeshirikiana na taasisi isiyo ya serikali kutoa taulo za kike kwa ajili wa kusaidia wasichana na wanawake, hili limekuwa na mafanikio na tangu nimekuja Tanzania," anasema.
Balozi huyo anasema, wanawake wa Tanzania wanajitihidi kuendelea kukuza uchumi wao, na kwamba serikali ya China na Tanzania nazo zinasaidia kuwawezesha kiuchumi ili kuwapa unafuu wa maisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED