ULAJI wa nyama ya nguruwe isiyoiva ipasavyo, ajali, uzazi pingamizi na mbung’o vimetajwa kuwa vyanzo vya kuenea kwa ugonjwa wa kifafa.
Pia imebainika kuwa wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa huo wako Ulanga, mkoani Morogoro na Hydom, Manyara.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania (TEA), kimechukua hatua kadhaa ikiwamo kuanzisha mradi wa kituo cha mafunzo ya tiba saidizi na ujuzi huko Mahenge wilayani Ulanga.
Bingwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu, Dk. Patience Njenje, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na vyombo vya habari kuhusu Siku ya Kifafa Duniani, itayaoadhimishwa Februari 10, mwaka huu.
“Duniani kote kifafa ni ugonjwa wa kudumu wa ubongo unaoathiri takribani watu milioni 60, huku ukiathiri watu 34-76 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaoongezeka kila mwaka, ukiwa na wastani wa uwiano wa asilimia 0.5 hadi moja.
“Nchini Tanzania athari ya jumla ya muda wote ni asilimia mbili. Afrika ina idadi kubwa ya walioathirika ikiwa ni kati ya watu 20 hadi 58 kwa kila watu 1000. Utafiti uliopita na wa sasa umegundua kuwa takribani watu milioni moja wanaishi na kifafa nchini. Mahenge huko Ulanga na Hydom wilayani Mbulu kuna wagonjwa wengi zaidi,” alisema.
Alisema maeneo ambayo yana idadi kubwa ya wagonjwa, sababu mojawapo ni za kijiografia zikiwamo kuwapo maambukizi kutokana na nzi aina ya mbung’o Pamoja na Hydom ambako kuna ulaji zaidi wa nyama ya nguruwe.
“Tanzania ni moja ya nchi zenye baadhi ya vijiji vyenye idadi kubwa ya walioathirika hadi kufikia watu 37.5 kwa kila watu 1000, ikiwa na watu 73 hadi 111 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaoongezeka kila mwaka.
“Kitimoto (nyama ya nguruwe) isipoiva ipasavyo, husababiosha minyoo ambayo husafiri hadi kichwani na kuziba damu kupita ipasavyo. Uzazi pingamizi, yaani mjamzito anapata tabu sana wakati wa kujifungua. Ajali ni sababu nyingine na wagonjwa wengi ni vijana, pengine mtoto alidondoka akiwa mdogo na kapata uvimbe baadaye anaanza kupoteza fahamu,” alisema.
Dk. Njenje, alisema yako mafanikio baada ya matokeo ya sasa ya utafiti kuonesha kupungua kwa idadi ya waathirika kutoka zaidi ya 70 hadi 20 au 15 kwa kila watu 1,000 na waathirika wapya kutoka zaidi ya 70 hadi karibia 50 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka katika baadhi va maeneo nchini.
“Kwa sasa kiwango cha vifo kwa wagonjwa kimeshuka kutoka kiwango kikubwa cha mara sita zaidi hadi mara nne, ikilinganishwa na kiwango cha vifo kwa watu wote. Wenye kifafa ni watu wenye umri mndogo wakiwa na wastani wa umri wa miaka 15.4 hali ambayo imebakia sawia na matokeo ya miaka 60 na 32 iliyopita,” alisema.
Dk. Njenje alisema asilimia 60 ya watu wenye kifafa huenda kituo rasmi cha kutolea huduma za afya kwa wastani wa mwaka mmoja kutoka degedege la kwanza.
Ni asilimia tano hadi 10 tu ndio hupata dawa sahihi na za mara kwa mara, hivyo pengo la ugunduzi na matibabu likibakia kubwa na mwenendo unaopungua katika maeneo baadhi kutoka asilimia 100 miaka 60 iliyopita hadi 95 miaka 30 iliyopita na kwa sasa ni takribani asilimia 50.
“Watu wenye kifafa walio kwenye umri wa kuoa au kuolewa, asilimia 67 hawajaoa au kuolewa. Kati ya asilimia 33 waliooa au kuolewa wana viwango vikubwa zaidi vya talaka. Karibu asilimia 24 ya watu wanaoishi na kifafa ni walemavu, kutokana na sababu zinazotokana na au kama matokeo ya dalili za kifafa (kukakamaa maungio kutokana na kuungua, makovu, majeraha ya kichwa,” alisema.
“Kwa sasa hatuna vituo rasmi vya tiba saidizi kwa watu wanaoishi na Kifafa isipokuwa vituo vitatu, vinavyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali katika vituo vya Kanisa Katoliki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED