IKIWA ni takriban miaka zaidi ya 20 tangu kutokea ajali ya treni eneo la kati ya Stesheni ya Msagali na Igandu mkoani Dodoma, wakazi wa Mtaa wa Mathias, Kata ya Miyuji wamelilalamikia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuyatelekeza makaburi ya waathirika wa ajali hiyo, hata kutumika kama maficho ya vibaka.
Ajali hiyo ilitokea Juni 24, 2002 ambapo katika eneo hilo kuna makaburi ya watu 88 kati ya 288 wa ajali hiyo.
Nipashe imetembelea eneo hilo na kubaini makaburi hayo hayajafanyiwa usafi kwa muda mrefu na hivyo kuzingirwa na vichaka vikubwa vinavyotumika kama maficho ya uhalifu na kutishia hali ya usalama.
Mmoja wa wananchi hao, Hilary Mark amesema kuna vichaka vikubwa ambavyo vinatumika kama maficho ya vibaka na wavuta bangi.
“Wakati huu ambao mvua inanyesha, vichaka ni vikubwa, limekuwa ni eneo la watu kujificha kwa kuwa unapopita ni eneo tulivu, halina msongamano wa watu, kiusalama hali si nzuri maana halina ulinzi, amesema.
Ismail Israel, mwenye makazi jirani na eneo hilo, amesema serikali za mitaa na TRC ambao wana wajibu wa kusimamia eneo hilo wamejisahau eneo hilo.
Mkazi wa Ipagala, Gersha Muhango ameomba watu wenye mamlaka kuliangalia eneo hilo na si kutekeleza makaburi hayo.
“Eneo hili wenzetu wamehifadhiwa sisi tulio hai, wajibu wetu ni kulifanyia usafi na si kuliacha na kuhatarisha usalama wa wananchi,” amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Sikuzani Daudi, amesema vitu mbalimbali vilivyokuwapo ikiwamo kichwa cha treni kilichotengenezwa kwa chuma, viliibwa.
“Yaani eneo hili wezi wanaiba huko wanakimbilia humu, ninashauri eneo hili liwe na ulinzi na tulihifadhi kama kumbukumbu ya wenzetu waliofariki dunia na tuwe tunawaombea kama ambavyo inafanyika kumbukumbu ya watu waliofariki dunia kwenye ajali ya meli ya MV Bukoba," amesema.
Akizungumzia malalamiko hayo, Msimamizi wa eneo hilo, Athuman Mamuya, amesema kipindi hiki vichaka vimekuwa vikubwa kutokana na mvua inayonyesha. Msimu wa mvua utakapoisha kuanzia mwezi Mei watafanya usafi.
“Pia kabla ya msimu wa mvua kuanza mwishoni mwa mwaka, tunarudia kufanya usafi huu, huu ndio utaratibu wetu wa kufanyia usafi eneo hilo," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED