Umoja wa Walimu Wasio na Ajira nchini (NETO) umewataka walimu wanaojitolea kuacha mara moja kazi hiyo ili kuonesha dhahiri uhitaji wa ajira katika sekta ya elimu na kulazimisha serikali kuchukua hatua za haraka.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa NETO, Daniel Edgar, amesema kuwa kuendelea kwa walimu kujitolea kunatoa taswira potofu kwa serikali kwamba kuna walimu wa kutosha nchini, ilhali baadhi yao wanalipwa kiasi cha Sh.70,000 kwa mwezi, huku wengine wakifanya kazi bila malipo yoyote.
"Tunawaomba na kuwataka wanachama wa NETO na walimu wote wasio na ajira kuacha mara moja kujitolea katika shule za serikali," amesema Edgar.
Aidha, Edgar ameitaka serikali kutoa ajira kwa wahitimu wa ualimu waliomaliza masomo yao kati ya mwaka 2015 na 2024 bila masharti yoyote, akipinga utaratibu wa sasa wa kuwafanyia usaili. Amesisitiza kuwa kundi hili lina haki ya kuajiriwa kwani wengi wao bado hawajapata nafasi ya kufanya kazi rasmi.
Katika hatua nyingine, Edgar ameiomba serikali kusimamia upangaji wa mishahara katika taasisi za elimu binafsi, akieleza kuwa kwa sasa kuna tofauti kubwa katika malipo ya walimu wa taaluma moja kulingana na ngazi tofauti za elimu. Ameeleza kuwa hali hii inahitaji uangalizi wa serikali ili kuhakikisha mshahara unalingana na kiwango cha elimu cha mwalimu, jambo litakalosaidia kuongeza weledi na motisha kazini.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NETO, Agnes Japhet Mpundi, ameonya kuwa ikiwa changamoto ya ajira itaendelea, elimu inaweza kugeuzwa kuwa chachu ya uhalifu. Amebainisha kuwa vijana waliosoma wanaweza kujikuta katika mazingira magumu yanayoweza kuwasukuma kwenye vitendo vya uhalifu iwapo hawatapata ajira kwa wakati.
Mpundi amehoji sababu za serikali kushindwa kutoa ajira kwa walimu licha ya ongezeko la mapato katika awamu ya sita, akilinganisha hali hiyo na kipindi cha utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo walimu waliweza kuajiriwa kwa mkupuo hata wakati ambapo mapato ya taifa yalikuwa madogo zaidi.
NETO imesisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kuchukua hatua za dharura kuhakikisha walimu waliomaliza masomo yao wanapata ajira rasmi ili kuboresha sekta ya elimu na kuzuia athari mbaya zinazoweza kutokana na ukosefu wa ajira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED