RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka wazi msimamo wake kichama na kiserikali, akionesha hana wa kumkumbatia, mwelekeo wake mkuu ni kila mtendaji wake kuwajibika.
Katika ujumbe wa aina yake, unaobeba ishara ya itikadi ya uongozi wake, Rais Samia ametumia fursa hiyo kutoa tahadhari ya kiutendaji kuanzia kwenye chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako yeye ni mwenyekiti hadi serikalini akiwa na itikadi 'mimi ni mtu wa wote'.
Ilikuwa kwenye tukio la jana la kuapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni serikalini, akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na naibu wake, Anamringi Macha, katika cheo kama hicho mkoani Shinyanga.
Kauli hiyo ya kipekee ya Rais Samia aliitoa Ikulu katika hilo, ambalo mbali na wakuu wa mikoa, pia alikuwapo Christina Mndeme ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Rais alitafsiri kwa kina msimamo wake kiutendaji na nyendo za kuwajibika kwa watendaji wote serikalini, hasa wanaowajibika kwake moja kwa moja.
Katika hotuba yake, Rais Samia aliweka wazi sababu za uteuzi wa kila mkuu wa mkoa na kutoa maelekezo mahususi na ya jumla kwa wateule wote, akiwa na msisitizo amewateua pasi na kuangalia makundi waliyonayo.
“Mabadiliko hayo wengine wamehamishwa na kuondolewa na si kwa kulenga mtu, bali kupanga safu nzuri kuelekea mbele. Wale mliobadilishwa nendeni mkasome vituo vyenu vipya, na uende inavyotakiwa.
"Wakati mwingine uliyebadilishwa ni kwa sababu ulipokuwapo changamoto ni chache, tunakupeleka kwenye (changamoto) nyingi tukiamini unaweza. Wakati mwingine ni nyingi na wewe ni mwepesi, tunampeleka ambaye ataweza. Ni mabadiliko ya kawaida, nendeni kufanya kazi.
“Mwanzo nilipoanza kuwaapisha wakuu wa mikoa niliwaambia mnatarajia ningewachagua kwa makundi, lakini mimi kama Samia sina kundi.
"Mkijitizama humo, makundi mnayoyajua wote mmo humo ndani, ninachotaka mimi Watanzania kwa pamoja tufanye kazi, tusogeze nchi yetu mbele, sina kundi.
“Sasa wale wanahoji ‘identify’ (kujitambulisha) huyu ni wa mama huyu siyo wa mama, mimi mama nina watoto wote, wote wangu ninalea. Anayefanya vizuri wangu, anayefanya vibaya wangu, mwingine nitampa zawadi na mwingine nitamchapa mikwaju.
"Na wapo ninawachapa, ninawaweka nje, akishapata adabu yake ninamwambia njoo tufanye kazi. Kama makundi yenu huko, mimi hayanihusu, ninataka tufanye kazi 2024 na 2025 tuvuke vizuri,” alisema.
KUVUNJA MIKATABA
Rais Samia pia alitoa angalizo kwa viongozi kutumia vibaya nafasi zao kwa kuvunja mikataba kwa njia ambazo si za kisheria na hivyo kusababisha serikali kushtakiwa na kuingia gharama kubwa za kulipa fidia.
"Tunalipa fedha nyingi sana kwa kuvunja mikataba ovyo, mtu hajawekeza hata shilingi kanyang’anywa ardhi, unaletewa bili hiyo 'lipa umekiuka Katiba na sheria, Dola 300 lipa'.
"Uvunjaji mikataba ufuate taarifa, vinginevyo DC (mkuu wa wilaya) na RC (mkuu wa mkoa) mnatutia hasara sana. Inawezekana umeenda mahali mtu anaudhi, lakini fuata taratibu kuvunja. Wengine ni matapeli kaingia, kategesha anakukasirisha ili afanye yake,” alifafanua.
WASIOWAJIBIKA
Rais Samia alisema kuwa kila mwezi anapokea ripoti ya utendaji wa kila kiongozi, akibainisha kuwa vipimo vya wakuu wa mikoa ni pamoja na kuongeza mapato.
“Wizara ya Fedha walinipa taarifa ya mapato, matumizi na madeni na kuonesha makusanyo ya serikali ni asilimia 97.7, lakini TAMISEMI makusanyo yako kwenye asilimia 60 hadi 70 kwa baadhi ya halmashauri na nyingine ziko kwenye 50, lakini 15 ziko chini ya asilimia 50 na kuwataka wajitazame namna ya kupandisha.
“Katika kupandisha makusanyo si kwenda kuwabinya wananchi, kuna maeneo mengi yameachiwa zinaweza kukusanywa. Tunakwenda kupunguza kwa ajili ya huduma za kijamii; elimu, afya na maji, ili fedha zirudi TAMISEMI, lazima kukusanya.
“Ninataka mkasimamie mifumo ya ukusanyaji, watu wanaiba fedha, watu wote, RC, DC mpo? Kuna mitandao inachepusha fedha za halmashauri, mkoa, kuna mtandao wa serikali unakwenda sambamba na wa wizi, watu mpo mnaangalia. Ninashukuru Mbeya wamekuwa wa kwanza kutuambia, tumeona hebu angalieni na kwingine, tunafuatilia.
“Mtandao upo na unaenda, wanaambizana na unachepusha fedha nyingi sana. Lakini mnakaa huko 'barabara zimeharibika El-Nino tunaomba fedha hizi', zinatoka wapi? Serikali hatuchapishi fedha, bali tunakusanya kodi huko na huku kwenu mkiziachia zipotee hizi za huku zitazidiwa, tuna miradi mikubwa ya kitaifa, kuna mabwawa, reli.
“Huko kwenye huduma za kijamii tumefanya vya kutosha, sasa tunakwenda kupunguza fedha labda mkusanye. Lakini halmashauri zitapewa fedha kutokana na makusanyo yake na watapewa kwa kadri ya kukusanya, wakipiga kelele nitafanya tathmini ya utendaji wako (kiongozi)," alihadharisha.
MIGOGORO YA ARDHI
Rais Samia alisema migogoro ya ardhi imekuwa mingi, watu hawana raha, kuna wababe wanajifanya maofisa ardhi wanawanyang’anya, akiagiza viongozi kusimamia haki za watu.
“Ninafurahishwa na juhudi za sasa za Wizara ya Ardhi kupita, kusikiliza kero na kuzitatua palepale, lakini waziri ni mmoja na timu yake wanaburuza wanakwenda, angalau wameanza na hawawezi kwenda kila mahali, bali serikali (viongozi) wafuatilie.
“Wakati huu tulionao uchaguzi wa serikali za mitaa ndio wakati wa kusababisha migogoro ya ardhi, mtu akiona ameharibu upande mmoja, anajenga mazingira linakatwa eneo anajisogeza na kijiji kinasajiliwa na wakifanya tathmini hakikuwapo na kimesogezwa kwenye hifadhi, wilaya au mkoa mwingine.
“Ramani zilivyokuwa kipindi kilichokuwa wakati wa uchaguzi hakuna kuongeza kijiji wala nini. Huu ndio mtindo wa madiwani, wakishavurunda huku wanakata upande mwingine, nendeni kasimamieni," aliagiza.
Pia aliwataka viongozi hao kuchunga ndimi zao kwa kuwa wakati mwingine zinachangia migogoro ambayo ni kuminya haki za watu, watambue wako kwa ajili ya kusimamia haki za watu.
MIKOPO YA 10%
Rais Samia pia alisema suala la mikopo ya halmashuari wanaendelea kulimalizia ili kuwa na utaratibu mzuri, watu wasipate shida. Alisema kuwa hata mwaka huu wa fedha (2023/24) kuna fedha ilishaidhinishwa, ipo kwenye mfuko ikisubiri muundo mpya.
Alisema makusanyo yanapaswa kuendelea na ni lazima wadaiwa sugu washughulikiwe, lakini akawa na angalizo kwamba itafika mahali watashindwa kwa sababu waliochukua fedha ni madiwani na wenyeviti wa halmashauri ambao waliunda vikundi feki vilivyopewa majina na kuundiwa miradi hewa na kupewa fedha.
SUKARI, MIGOGORO
Mkuu wa Nchi pia aliwataka wakuu wa mikoa kushughulikia aliowaita "watukutu" na kuacha kula nao ili kusaidia wananchi wapate sukari. Kama kuna mkoa bidhaa hiyo haipatikani na ipo nchini, watakutana kwenye tathmini ya mwezi.
“Ninapata taarifa za ajabu ajabu, nyingine mnajihatarishia maisha wenyewe. Mungu awalinde. Jitambueni. Uhusiano mwema sehemu ya kazi, mimi ninashangaa RC na DC haziendi huyu na huyu, kama binadamu kila mtu alizaliwa kwao na makuzi ya kwao ila wote tumepita shule.
"Kama ya nyumbani hayaendani na uliyemkuta, basi angalieni yale ya jumla, mnagombana kwa kipi? Ukifuatilia ni mamlaka, fedha na mali ndivyo wanavyogombania.
“Wabunge wakija na hayo huwa ninawaambia 'hapana'. Kama unafanya vizuri jimboni kwako hakuna wa kukuondoa, kama hufanyi vizuri unataka kubebwa hilo halipo.
"Ila kuna visa RC anampangia mwenzake mbunge mwingine badala ya kumwita ambaye hamwendi vizuri na kuelezana maeneo ya utawala, kuna ambao hawataki kusimamiwa na wanaojiingiza kwenye yasiyowahusu,” alionya.
RC NI RAIS
Rais Samia alisema lengo ni kuwakumbusha dhamana waliyonayo ni kwa kuwa mkuu wa mkoa ni mwakilishi wa Rais katika kipande cha ardhi alichoko, kwa maana ndiye Rais wa huko.
"Rais wa Tanzania mvua ikinyesha hukuna usingizi, unajiuliza wananchi wangu wa wapi wataamka wamezama, wapi nitasikia daraja limeporomoka, jua likitoka hulali je, wakulima watapata chakula? Vyanzo vya maji viko salama kweli, na ninyi mnatakiwa kuwa hivyo.
“Nimeona visa vingi hadi aje waziri mkuu azunguke huko akafungue maghala yaliyofungwa na RC mpo, na ninyi mnawaapisha DC ambao wamekatiwa kipande cha ardhi, lakini mambo hayaendi. Ninawakumbusha ninyi ndio marais wa eneo lile, shida yoyote ni yako," aliagiza.
MTWARA
Rais Samia alisema amempandisha cheo Kanali Patrick Sawala kutokana na kazi nzuri aliyofanya akiwa mkuu wa wilaya, huku akibainisha kuwa Mkoa wa Mtwara unapakana na nchi jirani, hivyo ahakikishe wanafanya vikao vya kujadiliana kupunguza changamoto za mpakani na kukuza biashara baina ya pande zote.
“Nenda kasimamie uzalishaji wa zao la korosho, mtangulizi wako alifanya vizuri, lazima kusimamia usafirishaji, tumeamua korosho yote isafirishwe kutoka Bandari ya Mtwara hatujapata lawama kwenye soko la dunia, tunapoamua korosho ije Dar es Salaam kuna mambo mengi yanafanyika, ila ikisafirishwa moja kwa moja tunapeleka zao lenye sifa,”alisema.
Aliongeza kuwa serikali imeanzisha kongani ya zao la korosho na ni muhimu kusimamia vyema ili kutoa ajira kwa wingi, huku akieleza bei nzuri ya zao mbaazi na ufuta inapaswa kwenda sambamba na usimamizi mzuri wa serikali.
TABORA
Alisema amemtoa Paul Chacha kutoka mkuu wa wilaya kuwa mkuu wa mkoa kutokana na kufanya vizuri huku akimtaka asimamie vyema mazao ya kilimo, hasa tumbaku na pamba pamoja na kutatua changamoto ya uharibifu wa mazingira.
Pia alimwagiza kusimamia zao asali ili wananchi wapate ajira na kusimamia mradi wa umwagiliaji eneo la Nala ili wananchi waachane na kilimo duni ndani ya mkoa huo.
Alisema TAMISEMI inatathmini wakuu wa mikoa na wilaya ili kujua wanaofanya vizuri na wanaofanya vibaya. Kwa Chacha, ripoti nzuri ilitolewa na ndio sababu wamempandisha.
SONGWE
Rais Samia alisema Chongolo anaijua vyema Songwe na matatizo yaliyoko huko tangu akiwa CCM. Inaunganisha nchi na Zambia kupitia Mpaka wa Tunduma ambako kuna shughuli nyingi za kiuchumi na uhalifu wa kiuchumi kama ukwepaji kodi, ubadilishanaji fedha isivyo halali.
“Kuna DED wa upande ule mzuri kaongeza mapato ya serikali, nenda kasaidiane naye pale Tunduma panaweza kuendesha mkoa na mkachangia serikali. Kuna matatizo ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), nenda kawasaidie wafanye kazi zao vizuri wakiwa pale.
SHINYANGA
Mkuu wa Nchi alisema Anamringi Macha ana uzoefu mzuri ndani ya chama na maeneo mengine, ametulia na amekua; atafanya kazi nzuri, akimtaka kusimamia vyema uzalishaji pamba na kupandisha ari ya wananchi kujiletea maendeleo.
“Pale (Shinyanga) kuna mabwanyenye, kulalalala kidogo, kuna jamaa zangu wengi waarabu kidogo, wengi kazi 'mzigo mzito mpe mnyamwezi' ila sio wengine , nenda kasimamie watu wapate ari ya kufanya kazi na kujiletea maendeleo, kufuatilia kongani ya Buzwagi hasa kwa madini, hatujawahi kuwa na ya aina hii, nenda kaisimamie iwe na mafanikio,” aliagiza.
WALIOHAMISHWA
Rais pia alisema Ruvuma hakuna changamoto nyingi kama Mtwara ila wakikosa mbolea, ikizingatiwa kuna tatizo la kiusalama mpakani, inakuwa shida.
“Ninadhani damu ya Peter (Serukamba) kule Singida haikuiva vizuri sana na viongozi walipo, vineno vineno vingi, nikijua Peter ni mtendaji mzuri sana, alikuwa anajaribu kurekebisha mambo wengine hawataki kurekebishwa, nikaona nikimwacha twende naye mpaka kule mbele kwenye kazi zetu zile, wanaweza kuharibiana.
"Halima (Dendego) wewe ni mama unaweza kulea, pale kuna watu wa kuelelewa kama ninavyowalea ninyi, nawe nenda kalee Singida, Singida ni ndogo lakini ina mambo yake," alisema.
Rais Samia alisema Serukamba anakwenda Iringa ambako kuko vizuri, hakuna changamoto nyingi na anadhani ataelewana nao vizuri; akiona anakwazwa amtafute Mtaka jirani yake (Mkuu wa Mkoa wa Njombe) atamwonesha njia ya kupita.
Kwa upande wa Balozi Batlida Buriani, Rais Samia alisema aanaamini atakwenda nao vizuri, akisisitiza kuwa waziri alikuwa anatumia nguvu, "mnyapara sana" na kumtaka asikubali wamwendeshe, lakini usibishane na wananchi wa Mkoa wa Tanga alikohamishiwa, bali asimame nao vizuri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED