MSHAMBULIAJI wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Pyramids FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, Fiston Mayele, amesema lolote linawezekana kuhusiana na uamuzi wa kujiunga na Simba katika msimu ujao wa 2024/2025.
Mayele alijiunga na Pyramids mwaka jana baada ya kuichezea Yanga kwa mafanikio ambapo msimu uliopita aliisaidia kucheza fainali za mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mshambuliaji huyo amekuwa akihusishwa kutakiwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao ili kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa ni tatizo linalowasumbua zaidi Wekundu wa Msimbazi.
Akizungumza baada ya kutembelea kambi ya Simba nchini Misri ambayo jana usiku iliwakabili wenyeji, Al Ahly katika mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mayele alisema mpira ni kazi yake na muda utakapofika kila kitu kitawekwa wazi.
"Kwa kweli tumuombe Mungu, tumalize msimu, na Inshaa Allah chochote kinawezekana," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo wa zamani wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mkongomani huyo alisema amefanikiwa kuitazama Simba katika mashindano ya kimataifa na kuona ina tatizo katika safu ya ushambuliaji ambayo ingekuwa vyema, ilikuwa na uwezo wa kuamua matokeo kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam.
Alisema katika mashindano makubwa safu ya ushambuliaji ndio huamua matokeo kwa sababu michezo hiyo ni ya kutumia kila nafasi zinazopatikana.
"Mimi kama mchezaji niliangalia mechi ya kwanza Tanzania, wenzangu walipambana, Simba walitengeneza nafasi, lakini hawakuzitumia vizuri. Siongei hayo kwa sababu mimi ni mshambuliaji bali kwa kuwa nimeangalia mchezo wa kimataifa,” Mayele alisema.
Nyota huyo alisema Al Ahly ya msimu huu si ile yenye makali kama ilivyokuwa zamani kwa sababu imetumia wachezaji wale wale kwa muda mrefu.
"Al Ahly wale wa zamani si wa sasa, unajua wao hawajabadilisha wachezaji, wachezaji ni wale wale wa zamani, wao ni binadamu, wanachoka, wanacheza mashindano mengi, ...kuna wachezaji wanapaswa kuamua matokeo, kuna Chama (Clatous)," aliongeza mshambuliaji huyo.
Kutokana na safu yake ya ushambuliaji kutofanya vyema, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, alilazimika kutumia siku tano baada ya mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali kuwanoa mastraika kwa ajili ya mchezo wa jana usiku.
Benchikha aliandaa dozi maalumu kwa lengo la kutumia vyema kila nafasi itakayopatikana na hatimaye Simba kufikia malengo yake.
Katika kuboresha safu ya washambuliaji ya Simba, wakati wa dirisha dogo iliwasajili Fred Michael na Pa Omar Jobe, ambao bado hawajaonyesha makali yanayotakiwa na kikosi hicho.
Simba pia inaamini bado inaweza kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo linashikiliwa na watani zao, Yanga huku pia Azam FC ikiwa kwenye vita ya kumaliza msimu wa 2023/2024 katika nafasi mbili za juu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED