Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Geita kwa tuhuma za kuanzisha vurugu, kuwapiga walimu na kuharibu mali za umma, wakishinikiza kurejeshwa kwa mwanafunzi aliyefukuzwa baada ya kukutwa na simu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro, amethibitisha kushikiliwa kwa wanafunzi hao leo, Februari 21, 2025, akieleza kuwa jeshi hilo lililazimika kutumia nguvu ya kadiri kuwadhibiti wanafunzi hao waliokuwa wakifanya vurugu usiku wa Februari 20, 2025.
Maro amesema vurugu hizo, ambazo zilihusisha kuwashambulia baadhi ya walimu na kuharibu mali za shule, zilisababishwa na tukio la kufukuzwa kwa mwanafunzi wa kidato cha sita aliyekamatwa na simu shuleni, kinyume na sheria za shule hiyo.
"Wanafunzi hawa 30 tunawashikilia na tunaendelea kuwahoji kuhusu vitendo vyao vya vurugu. Usiku wa tukio, saa mbili usiku, walianza kufanya fujo baada ya mwenzao, Brighton Philipo, kukutwa na simu ya mkononi kinyume na taratibu za shule," amesema Maro.
Ameongeza kuwa Philipo alipewa adhabu ya kusimamishwa masomo kwa muda wa siku 73, hali iliyozua taharuki miongoni mwa wanafunzi na kupelekea vurugu, wakidai kuwa hakutendewa haki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED