Chebukati afariki dunia hospitalini Nairobi

By Enock Charles , Nipashe
Published at 12:38 PM Feb 21 2025
Wafula Chebukati
PICHA:MTANDAO
Wafula Chebukati

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wafula Chebukati, amefariki dunia jana katika hospitali ya Nairobi alikokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Chebukati alihudumu kama mwenyekiti wa IEBC kwa muhula mzima wa miaka sita ambapo alisimamia Uchaguzi Mkuu mara mbili katika nchi hiyo.

 Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, Chebukati amefariki dunia jana Saa 11 jioni alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi. 

 Mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC alikuwa amelazwa katika hospitali akitibiwa kwa takriban wiki moja katika chumba cha wagonjwa mahututi. Imeelezwa kwamba awali Chebukati alikuwa akitibiwa nyumbani lakini alipelekwa hospitalini baada ya hali kuwa mbaya. 

Chebukati alihudumu kama mwenyekiti wa IEBC kwa muhula mzima wa miaka sita na alistaafu Januari 2023. Aliongoza uchaguzi wa 2017 ambapo rais wa zamani Uhuru Kenyatta alitangazwa kumshinda mgombea urais wa upinzani, Raila Odinga  na pia Uchaguzi wa 2022 ambapo Rais William Ruto alitangazwa kumshinda Raila Odinga.