Kamati Bunge yashtushwa ongezeko matumizi dawa za kulevya za kemikali

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:49 AM Feb 06 2025
Dawa za kulevya.
Picha: Mtandao
Dawa za kulevya.

KAMATI ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imebaini ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya zenye kemikali bashirifu nchini hasa aina mpya ya NPS ambazo zina viwango vikubwa vya kilevi mara 50 hadi 100 ikilinganishwa na dawa zingine.

Kutokana na hali hiyo, Bunge limeazimia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini ishirikiane na Taasisi ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwango (TBS) na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD), kudhibiti maduka ya dawa za binadamu kujihusisha na uuzwaji wa kemikali bashirifu nchini.

Akiwasilisha jana bungeni taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Joseph Mhagama, alisema kamati imebaini kwa mwaka 2023 Mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya nchini ilifanikiwa kuzuia uingizaji nchini wa kemikali bashirifu kilogramu 157,738.55 na kukamata kemikali bashirifu zenye ujazo wa lita 22,682 kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2024.

“Changamoto ya ongezeko la matumizi ya kemikali hizi bashirifu ‘NPS’ zina viwango vikubwa vya kulevya mara 50 hadi 100 ukilinganisha na dawa za kulevya zinazodhibitiwa kimataifa na hupelekea matatizo makubwa ya afya na athari za magonjwa mbalimbali ikiwamo utegemezi na uraibu usioponyeka kirahisi, magonjwa ya akili, moyo, mfadhaiko, kifafa na vifo vya ghafla kwa mtumiaji,” alisema.

Alisema Bunge linaazimia serikali ihakikishe elimu inatolewa kuhusu uwapo wa aina hiyo ya NPS na madhara ya kemikali hizo kwa jamii.

“Kamati inaishauri Mamlaka iendelee kudhibiti na kupambana na uingizwaji wa dawa za kulevya nchini na iendelee kuzishirikisha mamlaka nyingine za serikali kama TBS, TMDA na MSD ili kuhakikisha kwamba, taasisi hizi zinashirikiana kwa pamoja kudhibiti uchepushaji wa kemikali na dawa halali kutumika kinyume na matumizi yaliyokusudiwa (dawa za kulevya),” alisema.

Pia, alisema Bunge linaazimia serikali iongeze bajeti ya mamlaka ili kujenga vituo vya matibabu na msaada wa kisaikolojia kwa waraibu wa dawa za kulevya hadi ngazi ya mkoa.

“Na kuimarisha udhibiti wa uingizwaji wa dawa za kulevya nchini kwa kutumia mifumo ya kisasa katika sehemu za usafirishaji na upakuaji mizigo nchini,” alisema.

Alisema Bunge linaazimia serikali kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) na ikishirikiana na Asasi za kiraia nchini iwafikie wananchi wote nchini hasa waishio maeneo ya vijijini.

Kadhalika, alisema serikali iiwezeshe Tume ya kurekebisha sheria kwa kuitengea fungu la maendeleo ili kutekeleza jukumu la kufanya utafiti kwa sheria kabla hazijaletwa bungeni.

“Serikali ihakikishe kwamba inatenga Bajeti ya kutosha kwa Tume ya Kurekebisha Sheria ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema serikali iratibu utengenezwaji wa mfumo wa pamoja wa ulipaji kodi (mifumo ya kodi kusomana) kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini.

“Kuwapo kwa mfumo mmoja wa utoaji leseni za biashara nchini kwa wawekezaji wazawa na wa kigeni ambao utaratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania,” alisema.