DRC yaingia mtegoni, M23 yaanzisha mashambulizi mapya yatwaa mji wa madini

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:48 AM Feb 06 2025
DRC yaingia mtengoni, M23 yaanzisha mashambulizi mapya yatwaa mji wa madini
Picha: Mtandao
DRC yaingia mtengoni, M23 yaanzisha mashambulizi mapya yatwaa mji wa madini

Siku moja baada M23 kudhaniwa kuanza kutekeleza sitisho la vita kufuatilia taarifa ya awali, suala hilo limeoneka kuwa ni mtego dhidi ya Majeshi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hii ni baada ya M23 kufanya shambulizi la kushtukiza na kuchukua Mji wa madini katika jimbo la Kivu Kusini, wakati wakiendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa Bukavu.

Baada ya M23 inayotajwa kusaidiwa na Majeshi ya Rwanda kuuchukua mji wa kimkakati wa Goma  huko  Kivu Kaskazini, walitangaza kusitisha mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kuanza siku ya Jumanne. 

Hata hivyo sitisho hilo limeoneka kuwa mtego kwa DRC kutokana na mapigano makali yaliyoanza Februari 5, 2025 na kundi hilo likitajwa kuwa na washirika wake Wanyarwanda hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la AFP. 

M23 na majeshi ya Rwanda wameuchukua  mji wenye madini wa Nyabibwe, kilometa 100 kutoka  Bukavu na kilometa 70 kutoka uwanja wa ndege wa jimbo hilo.

Kuanzishwa kwa mashambulizi hayo mapya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kunakuja siku chache kabla ya marais wa Rwanda na Kongo kuhudhuria mkutano wa kilele wa mgogoro huo jijini Dar es salaam.

Msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya, alisema hatua ya usitishwaji wa vita upande mmoja ni uthibitisho wa kuwa ni njama za kundi hilo kufanya mashambulizi zaidi.

Katika tangazo lao M23 walisema "hawana nia ya kuchukua udhibiti wa Bukavu au maeneo mengine" lakini suala hilo limeoneka ni tofauti baada ya mashambulizi kuanza upya.