KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii kulikuwa na ushuhuda wa huduma ya choo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, ikiwamo kukosekana mahitaji na huduma muhimu kwa watumiaji wanaotozwa ushuru. Endelea na picha pana ya athari zilizoko na undani wake kitaalamu.
---
Kushindwa kulipa gharama ya huduma ya choo katika kituo hicho cha mabasi kumechangia baadhi ya watumiaji wake kujisaidia holela, ikiwamo kutumia chupa na kuzitupa, jambo ambalo ni hatari kwa afya na mazingira.
Waathirika wakubwa wa gharama hizo ni wale ambao kituo hicho ndiyo sehemu yao ya kujipatia kipato, wakijumuisha madereva wa matoroli na wafanyabiashara ndogo.
Sheria Ndogo za Vituo vya Mabasi na Maegesho ya Vyombo vya Moto za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo za Mwaka 2022 zinaelekeza adhabu kwa wanaokiuka sheria hiyo, wakiwamo wanaokwenda kulipa huduma ya choo na ushuru wa kiingilio getini.
Sheria inaelekeza "...matumizi ya vyoo na bafu kwenye vituo vya mabasi yatalipiwa kwa viwango vilivyoainishwa. Ni kosa kwa mtu yeyote kuingia katika vituo vya mabasi pasipo kulipia ushuru husika.
"Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya sheria ndogo hizi, atakuwa ametenda kosa na iwapo atapatikana na hatia na kama hakuna adhabu maalum iliyoainishwa katika kifungu kilichokiukwa, atatozwa faini isiyopungua Sh. 200,000 na isiyozidi Sh. milioni moja au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miezi 24 au vyote kwa pamoja (faini na kifungo)."
Hata hivyo, licha ya utozaji huo wa ushuru uliowekewa msisitizo wa kisheria, mwandishi wa habari hii amebaini huduma ya choo iliyoko katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, haikidhi viwango vya kiafya.
Hali hiyo inakinzana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 inayoelekeza "kila mtu anayeishi Tanzania, atakuwa na haki ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya."
Mtaalamu wa Mazingira, Dk. Felician Kilahama, anasema huduma ya choo ni ya msingi, akiwa na angalizo lingine kwamba iwapo kuna gharama za uendeshaji wa huduma hiyo katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama inavyoshuhudiwa katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, kuwe na vyanzo vingine vya mapato kuendesha huduma hiyo.
"Kuna mtu hiyo Sh. 200 ni kubwa. Uendeshaji huduma ya choo katika vituo vya mabasi uwe unachangiwa na vyanzo vingine. Sh. 200 unaona ni kidogo, lakini kuna ambaye hana kitu, hiyo kwake ni nyingi.
"Fedha si kila kitu lakini afya! Afya ikiwa duni, hata mwenye fedha utagharamika. Mambo yakiharibika, watu wakijisaidia ovyo, kipindupindu kikiingia, kitawakamata wote, watoto na familia yako.
"Iwapo sheria kali kwa wanaojisaidia katika maeneo ambayo si vyoo baada ya huduma hiyo kuwa bure kwa watu wote. Mtu akikamatwa aadhibiwe. Tujifunze unapokuwa na huduma kubwa ya umma, choo ni muhimu. Hata ukienda Mlimani City, choo ni bure, SGR (reli ya kisasa) choo ni bure, uendeshaji huduma ya vyoo katika maeneo hayo unagharamiwa kwa namna nyingine, si moja kwa moja mtu kulipia huduma ya choo," anashauri.
Umoja wa Mataifa (UN) katika kuadhimisha Siku ya Choo Duniani mwaka jana, ulibainisha katika tamko lake kuwa mtu mmoja kati ya watatu kote duniani, hapati huduma ya choo.
UN ilibainisha wastani uliopo duniani kwa ujumla -- mtu mmoja kati ya wanane hujisaidia hadharani, huku watu bilioni 3.6 hawana huduma hiyo, hivyo kusababisha magonjwa kama kipindupindu, kuhara, homa ya matumbo, maambukizi ya minyoo ya matumbo na polio.
Katika maadhimisho ya Siku ya Choo Duniani Novemba 19, 2023 aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy, aliagiza mikoa na halmashauri kutekeleza ukaguzi kwenye kaya, sehemu za jumuiya, maeneo ya biashara na taasisi zote kuhakikisha zinajenga na kutumia vyoo bora.
Pia alielekeza kusimamia vyema Sheria ya Afya ya Jamii na Sheria Ndogo inayohimiza ujenzi, matumizi ya choo bora kwenye ngazi ya kaya, taasisi na maeneo ya jumuiya.
Vilevile, Ummy alielekeza kuhakikisha mamlaka zinasimamia vyema matumizi ya vyoo kwa wasafiri wawapo safarini kwa kuhakikisha mabasi yanasimama kwenye maeneo rasmi, ikiwamo stendi za mabasi na vituo maalum na kupiga marufuku tabia ya wasafiri kujisaidia ovyo njiani, maarufu "kuchimba dawa".
UZOEFU TRC
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Shirika la Reli Tanzania (TRC), Fredy Mwanjala, anasema kwa wastani kwa siku moja watu maelfu, wakiwamo abiria 7,000 hufika kwenye stendi kuu ya usafiri wa reli ya kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam.
"Kuna idadi kubwa ya watu wanaofika kwenye kituo hiki cha Dar es Salaam kwa siku. Huduma za choo zinapatikana bure na vyoo wakati wote huwa vinafanyiwa usafi," anasema.
Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli uligharimu Sh. bilioni 50.9. Kilizinduliwa rasmi Februari 22, 2021 na Rais wa wakati huo, Dk. John Magufuli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED