MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amesema chama kitaendeleza falsafa ya maridhiano na wako tayari kuunganisha mawazo yanayotofautiana ili kuendeleza misingi ya amani nchini.
Aidha, amesema anawajua wapinzani na hawampi shida kwa kuwa nchi inaendeshwa kwa hoja na si nguvu yoyote.
Wasira pia ameshauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukagua ardhi iliyoporwa kinyume cha sheria kwa wanakijiji irudi kwa kuwa sera ya CCM inaelekeza watu wote wana haki ya ardhi bila kujali kipato chao.
Akizungumza jana jijini hapa kwenye hafla ya kumpokea Makao Makuu ya CCM, Wasira alisema maridhiano yaliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan yanakusudia kuendeleza kujenga nchi kuwa na umoja na amani.
“Sisi ni mfumo wa vyama vingi, tukitofautiana tuongee na ukienda kuongea huwezi kupata kila kitu wewe, huko si kuongea, ni kupora haki. Tunasema sisi CCM kwa kuwa tunathamini amani, tupo tayari kuunganisha mawazo yanayotofautiana ili kupata mwafaka wa kuendeleza nchi kwenye misingi ya amani," alisema.
Wasira alisema CCM inaamini katika ustahimilivu na kwamba mwenye matatizo aende wazungumze. Milango iko wazi.
“Usije ukaja na mambo ya no reform no election (hakuna uchaguzi bila mabadiliko), hiyo si ajenda. Ni amri. Sasa sisi watu wazima, tuna chama kikubwa zaidi Afrika, hatuko tayari.
"Tunasema twende kwenye uchaguzi, tumeshafanya reform na wenzetu waende kwenye majimbo, urais tumewapiga bao wakienda watashindwa.
"Tuwaambie ukweli tupo tayari kuzungumza na tupo tayari kuendesha uchaguzi huru na haki, wanasema serikali za mitaa kulikuwa na matatizo, tuseme ukweli zaidi ya nusu ya nafasi zilikuwa hazina wagombea wa upinzani," alisema.
Aligusia jinsi alivyokuwa akitajwa kwenye mitandao ya kijamii wakati wa mchakato wa kumpata Makamu Mwenyekiti wa CCM na kuona watanzania wakimtaja kuwa awekwe yeye ili apambane na hoja za wapinzani.
“Kushika dola na kushinda ni lazima, tuna wanachama milioni 12.5 ambao wamesajiliwa kwa mfumo wa kielektroniki na bado tunaendelea kusajili, huu ni mtaji wa ushindi kwa kuwa ninyi ni askari wa mbele kukivusha chama hiki. Tunawaacha wale wajukuu wa kuchezea ndevu za babu sisi tunashika dola," alisema.
ARDHI
Kuhusu ardhi, Wasira alisema ni haki ya watanzania kuwa na ardhi. Ni msingi wa maisha na ni sera ya CCM na kuna sheria inasema ukitaka ardhi zaidi ya ekari 25, wanakijiji wanapaswa kukutana na kuandika muhtasari na kupitia hatua zote hadi kutiwa saini na Rais.
"Kuna watu huko vijijini wana ardhi kubwa, hawana saini ya Rais, hawa ni wavamizi. Ninaomba niwaambie Wizara ya Ardhi ikague ardhi iliyoporwa kwenye vijiji kinyume cha sheria irudi kwa wanakijiji. Tatizo la rushwa duniani ni hilo, unapora halafu unahalalisha kwa rushwa," alisema.
Aliwataka wasiruhusu ardhi ikauzwa kama kanzu. Kuna hatari ya kusababisha watanzania kukosa mahali pa kuishi.
Awali Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai alimwomba Wasira amfikishie salamu Rais Samia itakapofika Oktoba wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dodoma imejipanga kuongoza kwa kura nyingi za Rais kutokana na maendeleo aliyowafanyia wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED