CHADEMA bado kwawaka moto

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 09:59 AM Jan 24 2025
CHADEMA bado kwawaka moto.
Picha: Nipashe Digital
CHADEMA bado kwawaka moto.

LICHA ya kupatikana kwa uongozi mpya, ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), bado kuna mnyukano wa chinichini unaendelea kwa makada wake ikiwamo waliokuwa wanawaunga mkono wagombea wa nafasi hiyo.

Jana asubuhi, kada wa chama hicho,  Godbless Lema, aliyekuwa upande wa Tundu Lissu, aliyeibuka mshindi nafasi ya Mwenyekiti, akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds, alisema mara ya kwanza alipoona misuguano imekuwa mikali aliwatuma watu wamwambie aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ajitoe katika kinyang’anyiro hicho ili alinde heshima yake lakini hakufanikiwa.

Alisema baada ya uchaguzi imekuwa tofauti, heshima yake imepanda zaidi kutokana na kile alichokiita amefanikisha uchaguzi wa haki, huru na uwazi.

Lema alisema Mbowe hekima ilimwongoza kwamba uchaguzi usipokuwa wa wazi hata akishinda itaharibu heshima yake na taswira ya chama. Alisema  taarifa ya kusimamia kura za Lissu ilikuwa ya kushitukiza huku akibainisha kwamba kampeni za uchaguzi huo zilikuwa ngumu kwake.

Alisema alitaka kukaa kimya na kutomuunga mkono yeyote lakini alishindwa kwa sababu aliona chama kinamhitaji Lissu na kwamba aliwashirikisha pia ndugu zake.

Pia alikumbusha kuwa aliwahi kuzungumza naye kuhusu kuondoka kwa waliokuwa makada, Dk. Willibrod Slaa, Zitto Kabwe na Prof. Kitila Mkumbo, hakukua na faida yoyote bali chama kilipata hasara.

Baada ya mahojiano hayo, wafuasi wa Mbowe walionesha kukerwa na kuandika mtandaoni huku wakitishia kueleza mambo mengi zaidi.

Wa kwanza kuandika ni Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema aliyeandika: “Kesho Mwenyezi Mungu akinijalia nitasema kwa kinywa kipana. “Taasisi ni muhimu sana! matusi na kejeli havijengi! kuishi ughaibuni havijengi,” alisema.”

Masaga Karoli, Mwenyekiti CHADEMA Mkoa Mbeya alimwomba Lissu awe mwenyekiti mpatanishi na muunganishi kama alivyokuwa Mbowe na asiwe na timu yoyote na akubali kuponya majeraha.

Mbowe katika matandoa wake wa X, aliandika: “Nimesoma neno la leo katika Kalenda ya KKKT kwenye Biblia kutoka Kitabu cha Yakobo 3 : 13 - 18. Limenirutubisha. Natamani nanyi mrutubishwe nalo. 

"Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aoneshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima. Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli. Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani.

“Maana popote palipo na wivu na ubinafsi, hapo pana fujo na kila aina ya uovu lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi;  inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki. Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.”

Baadhi  ya wafausi wake katika mtandoa huo, walitoa maoni yaliyoonesha ujumbe wake una ukakasi wakihusisha na matokeo ya uchaguzi. 

Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jocob,  ambaye alikuwa wakala wa Mbowe katika uchaguzi huo, aliandika: “Kwangu umekuwa si tu kiongozi wangu wa chama bali ni mwalimu, mwanafalsafa, mkufunzi, mzazi, mlezi na rafiki wa kweli. Wewe ni mfano wa kuigwa.

“Nashukuru kwa kuniamini na kunipa jukumu la kuwa mwenyekiti wa kampeni zako katika uchaguzi mkuu wa chama Januari 2025,”

Aliendelea kusema anajua ameona, amesikia na ameshuhudia hadi sekunde ya mwisho alivyosimama naye na alivyojitoa kwa hali na mali  kufanya jukumu lile lakini bahati haikuwa upande wao.

Aidha, alisema hakuwahi kufikiri au kudhani iko siku mwalimu wake wa siasa atampa yeye mwanafunzi wake kazi ya kusimamia kazi yake ya siasa.

“Hata hivyo, nachezwa na machale, ninavyokufahamu itakuwa kuna kitu ulitaka nijifunze kwenye majukumu yangu ya kusimamia kampeni zako.

“Funzo kubwa na la ajabu nitalikumbuka daima katika uchaguzi huu ni pale uliponieleza watu wako uliowapa jukumu la kufanya kampeni wasifanye jambo lolote bila idhini yako. Pia katika kila jambo tutakalofanya tusikiumize chama kwa namna yoyote,” alisema Jacob.

Alisema mapenzi yake kwa CHADEMA na wanachama wake yalimfanya akubali kubeba jukumu hilo zito na kwamba alistahili msaada wake hata kama dunia nzima ingemsaliti.

“Ndiyo maana nilipoona kura zetu hazijatosha sikuhitaji ruhusa yako kusaini fomu ya matokeo kuwa Tundu Lissu ni mshindi.

“Na nilipokujulisha matokeo ya uchaguzi kuwa wajumbe 482 walihitaji uwe Mwenyekiti wao na wajumbe 513 wameamua ukapumzike. Watu  wengine uliokuwa nao chumba cha VIP wakiwa wanalia  wewe ulinyanyuka ukanikumbatia kisha ukachukua simu yako ili kupongeza na kukubali matokeo kupitia ukurasa wako wa X.” alisema.

Taarifa za kuaminika zinaeleza baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wamekwama kwenye hoteli mbalimbali baada ya kutolipwa fedha za kujikimu, huku wengine mizigo yao ikishikiliwa hadi walipe fedha za malazi.