Kesi za ndoa, mirathi K’njaro, zaitisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:24 PM Jan 24 2025
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakipata huduma za msaada wa kisheria kutoka mawakili wa Ofisi ya Mwanamsheria Mkuu wa Serikali katika kliniki ya bila malipo inayoendelea mjini Moshi.
Picha: Godfrey Mushi
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakipata huduma za msaada wa kisheria kutoka mawakili wa Ofisi ya Mwanamsheria Mkuu wa Serikali katika kliniki ya bila malipo inayoendelea mjini Moshi.

OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imebaini idadi kubwa ya kesi zinazowasumbua vichwa, wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa, ni migogoro ya ndoa, mirathi, jinai na kukithiri kwa kesi zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza leo, Januari 24, 2025, kuhusu mwenendo wa Kliniki ya Sheria bila Malipo, inayoendelea viwanja vya stendi ya vumbi, jirani na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Moshi, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Joseph Shoo, amesema siku tatu za mwanzo wa kliniki hiyo idadi kubwa ya malalamiko yaliyowasilishwa ni kuhusu kesi hizo.

“Tangu tulipoanza kliniki hii, Januari 21 kuelekea kilele chake Januari 27 mwaka huu, mwitikio wa wananchi ni mzuri. Tumeweza kupokea malalamiko mengi yanayohusu masuala ya ardhi, mirathi, jinai, ndoa na masuala ya kijinsia.

….Baadhi ya malalamiko tuliyoyasikiliza, tumeyatatua hapa hapa na mengine tumeyachukua kwa hatua zaidi. Niendelee kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wajitokeze zaidi ili tuweze kuwahudumia, “amesema Wakili Shoo.

Kliniki hiyo ilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu Januari 21 mwaka huu.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakipata huduma za msaada wa kisheria kutoka mawakili wa Ofisi ya Mwanamsheria Mkuu wa Serikali katika kliniki ya bila malipo inayoendelea mjini Moshi.
Akizungumza baada ya kupata huduma kwenye kliniki hiyo, Mohamed Marandu, ameeleza kuridhishwa kwake na huduma pamoja na maelezo aliyoyapata kutoka kwa Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku akisema anaamini kliniki hiyo itawasaidia wananchi wengi kupata haki zao.

“Kupitia kliniki hii nimeweza kupata maelezo mazuri kuhusiana na suala langu la ardhi, mawakili wamenipokea vizuri na kunieleza hatua sahihi za kufanya ili niweze kupata haki yangu, nawashukuru sana kwa kuja na kutoa elimu hii,” amesema Marandu.

Kwa upande wake, Emiliana Maliwa, ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuendesha kliniki ya kisheria bila malipo kwa wananchi kwani ofisi hiyo imezingatia watu ambao hawana uwezo wa kuwalipa wanasheria katika kuwasimamia masuala yao ya kisheria ya aina zote ili waweze kunufaika na huduma hiyo.

Katika hatua nyingine, Isack Ngupa, ameiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufanya kliniki hiyo mara kwa mara na kupeleka huduma hizo za ushauri wa kisheria katika maeneo ya vijijini, ambako wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya kisheria hivyo kupelekea kupoteza haki zao.