Mtendaji wa kata aongoza wananchi ujenzi vyumba vya majiko, stoo

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 05:58 PM Jan 24 2025
Mtendaji wa kata aongoza wananchi ujenzi vyumba vya majiko, stoo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtendaji wa kata aongoza wananchi ujenzi vyumba vya majiko, stoo.

MTENDAJI wa Kata Suguti Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Boniface Dinda ameongoza wakazi wa kijiji hicho kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa majiko na stoo katika Shule za Msingi Suguti A na Suguti B.

Uchimbaji wa msingi huo ulifanyika jana, huku mtendaji huyo akiwashukuru wananchi hao, kwa kujitoa kuboresha miundombinu ya shule hizo.

Alisema kitendo cha wananchi hao kuacha kazi zao na kujitolea kufanya kazi ya umma, ni wazi wanajua wajibu wao.

Mtendaji huyo aliongeza kuwa kwa sasa Suguti ni makao makuu ya Halmashairi ya Wilaya ya Musoma, na kwamba wananchi hawana budi kuboresha miundombinu mbalimbali ya kijiji chao.

"Mmekuwa sehemu kubwa ya maendeleo ya kijiji hiki, kwani ujenzi wa majiko haya na stoo ni muendelezo wa kuwasaidia watoto wetu waweze kupata chakula cha mchana shuleni," alisema Dinda.

Aidha, mtendaji huyo alimpongeza Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Suguti, Joel Samson kwa jinsi anavyohamasisha na kutekeleza shughuli za maendeleo.