Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, leo Januari 24, 2025, ameshuhudia utiaji saini wa mikataba tisa ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) mkoani Shinyanga na wakandarasi.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ikihudhuriwa pia na viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza katika hafla hiyo, RC Macha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji, akisema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza upatikanaji wa maji vijijini na mijini, kufikia asilimia 70 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.
RC Macha amesema mikataba hiyo ya shilingi bilioni 4.8 itahusisha ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 16, ikiwa ni pamoja na vituo 18 vya kuchotea maji. Pia, miradi hiyo itapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji, kutoka asilimia 68 hadi 70.
Amewataka wakandarasi kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa weledi na kukamilika kwa wakati, huku akisisitiza ushirikiano na wananchi wa maeneo husika ili kuwapatia ajira. Pia aliagiza RUWASA kutoa ripoti ya maendeleo kila tarehe 15 ya mwezi ili kufuatilia changamoto na kuzitatua mapema.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Juliety Payovela, amesema miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita, ifikapo Juni 2025, na itatekelezwa katika maeneo ya Kahama, Kishapu, na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Amebainisha kuwa vijiji 51 kati ya 506 havijafikiwa na huduma ya maji, huku juhudi za serikali zikiongeza uchimbaji wa visima 20 kwa shilingi bilioni 1.2.
Changamoto zilizotajwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo ya Ushetu na Kishapu, na ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, amewataka wakandarasi kuhakikisha mabomba yanayotumika ni bora ili kuepusha upotevu wa maji kutokana na mabomba kupasuka. Mbunge wa Msalala, Idd Kasimu, amempongeza Rais Samia kwa juhudi za kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa kiwango cha juu, akisema asilimia 98 ya miradi ya maji katika jimbo lake imetekelezwa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amesifu utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwapongeza wakandarasi kwa uaminifu wao katika kazi.
Mnandi Mnandi kutoka Kampuni ya URSINO LTD aliishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi, akiahidi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kwa viwango bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED