Tanzania mwenyeji Kongamano la Kimataifa la Utalii wa Vyakula Barani Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:23 PM Jan 24 2025
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili na wakionyesha makubaliano waliosaini kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili na wakionyesha makubaliano waliosaini kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.

Tanzania na Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimesaini mkataba wa makubaliano utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 11 hadi 13, 2025.

Hafla ya utiaji saini imefanyika  kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana  na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa  jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chana amesema Tanzania inafuraha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo linalotarajia kukutanisha washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali  duniani na kwamba kupitia kongamano hilo Tanzania itajifunza kutoka mataifa hayo  namna wanavyofanya katika kukuza utalii wa vyakula.

“Kupitia Kongamano hili tunataka kuwajengea uwezo wapishi wetu jinsi ya kutengeneza aina tofauti za vyakula ili watalii wanapokuja waweze kufurahia vyakula vya nyumbani kwao lakini pia tunahitaji kuona ni fursa gani zitakazotokana na kongamano hilo ili tuweze kujifunza utangazaji utalii wa vyakula” Chana amesisitiza.

Chana amefafanua kuwa Tanzania na UN Tourism zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali kwa lengo la kukuza utalii.

“Miongoni mwa maeneo tunayoomba ushirikiano kwa sasa  ni katika masuala ya sera na ukuzaji ujuzi, Rasilimali Watu na  Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii” amesema Chana.

Katika hatua nyingine, Chana amesema Tanzania inatambua na kuthamini jukumu muhimu la Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) katika kuunda sera za kimataifa za utalii,kukuza utalii endelevu na kukuza ukuaji wa uchumi.

Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili amesema kuwa Shirika la Utalii Duniani limelenga kuitangaza Afrika kama sehemu ya utalii inayofikika sambamba na kutangaza utalii wa vyakula. 

Katika kufanikisha kongamano hilo, Pololikashvili amependekeza kwa Tanzania kutumia njia zote za  mawasiliano ili kulitangaza kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kutumia watu maarufu wenye ushawishi katika jamii na kuwatumia wapishi wa vyakula mbalimbali vya kiafrika.

“ Pia ningeiomba Tanzania kuhakikisha zoezi la upatikanaji wa viza pamoja na usafiri wa anga kwa ujumla linakuwa rafiki kwa waombaji wanaotarajia kusafiri kuja kwenye kongamano hilo” amesisitiza Pololikashvili.

Mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Balozi Ramadhani Dau, Balozi wa Tanzania nchini Hispania, Balozi, Ali Jabir Mwadini, Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Thereza Mugobi, Mjumbe wa Bodi ya TTB, Said Kamugisha na Afisa Balozi, Amos Tengu na sekretarieti ya  Shirika la UN Tourism.