Rais Samia: Walipakodi mjitahidi kulipa kodi kwa hiari, acheni dhuruma

By Miraji Misala , Nipashe
Published at 05:05 PM Jan 24 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha: Miraji Msala
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka walipakodi nchini kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuacha vitendo vya ukwepaji kodi ambavyo vinaathiri usawa wa ushindani sokoni.

Akizungumza jana Januari 23 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Mlipakodi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rais Samia alisema utoaji wa tuzo hizo unalenga kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari.

Rais Samia alisisitiza kuwa vitendo vya ukwepaji kodi siyo tu vinadhoofisha uchumi wa nchi bali pia vinakatisha tamaa walipakodi waaminifu. Pia aliwataka watumishi wa TRA kuhakikisha wanapambana na wale wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia stempu bandia kwenye bidhaa.

Rais Samia alisisitiza kuwa masuala ya kodi hayana mzaha na hakutakuwa na mtu yoyote atakayepata ruhusa ya kutolipa kodi. Aliwataka TRA kusimamia kwa uaminifu ukusanyaji wa kodi ili kupunguza utegemezi wa nchi kwenye misaada ya nje.

Rais Samia alibainisha kuwa serikali imelenga kuongeza idadi ya walipakodi badala ya kuwategemea wachache waliopo, kupitia kurasimisha sekta isiyo rasmi. Alisema, "Bajeti ya serikali ya shilingi trilioni 49.34 inategemea kwa asilimia 61.6 mapato ya kodi."

Pia alitangaza kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026, Tuzo za Mlipakodi za TRA zitabadilishwa na kuwa Tuzo za Rais ili kuonyesha umuhimu wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya taifa.

3

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi yanalenga kuwatambua na kuwashukuru walipakodi wa sekta mbalimbali kwa mchango wao. Aliainisha vigezo vya ushindi wa tuzo kuwa ni pamoja na rekodi nzuri ya ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati, matumizi sahihi ya mashine za EFD, na ushirikiano wa karibu na TRA.

Pia alisema TRA imefanikisha makusanyo makubwa ya kodi kwa kuvuka malengo ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kukusanya shilingi trilioni 16.528.

Kamishna Mkuu Mwenda aliahidi kuwa TRA itaendelea kutoa huduma bora, kupambana na magendo, na kusuluhisha migogoro kwa kushirikiana na walipakodi.