TANAPA yaja na "Valentine Weekend Gateway" ndani ya Kisiwa cha Saanane

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:34 PM Jan 24 2025
TANAPA yaja na "Valentine Weekend Gateway" ndani ya Kisiwa cha Saanane.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Busybee Cabins, limezindua rasmi kampeni ya "Valentine Weekend Gateway na TANAPA" Jijini Mwanza.

Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha Watanzania na wageni wa mataifa mengine kutembelea Hifadhi za Taifa msimu huu wa Sikukuu ya Wapendanao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo juzi, Kamishna wa Hifadhi za Taifa,Lyimo, alisisitiza dhamira ya TANAPA ya kuwafikia watu wengi zaidi kwa kutoa vifurushi vya gharama nafuu ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kutalii katika kipindi hiki maalum.

"Leo tunazindua kampeni hii kwa Hifadhi zote 21. Tunawahamasisha Watanzania wote kutembelea Hifadhi zetu, maana tumeandaa vifurushi rafiki vya bei nafuu vinavyomwezesha kila Mtanzania kumudu gharama za kutalii msimu huu wa wapendanao," alisema Kamishna Lyimo.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk. Tutindaga Mwakijambile, ambaye pia ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane, alieleza upekee wa kisiwa hicho kama kivutio bora kwa wapendanao.

“Kisiwa cha Saanane ni mahali pa kipekee kwa wapendanao. Kina mandhari tulivu, fursa za kupumzika, na shughuli mbalimbali za burudani zinazowapa wageni uzoefu wa kukumbukwa milele. Watalii watafurahia msitu wa kijani uliosheheni miamba mikubwa, wanyama kama Swala, Nyumbu, Simba, na Mamba, pamoja na ndege wa aina mbalimbali,” alisema Dk. Tutindaga.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Busybee, Baraka Nyororo, alielezea kwa kina ushirikiano wa kampuni yake na TANAPA katika kuandaa tukio hilo, akibainisha kuwa Februari 15, 2025, inatarajiwa kuwa siku ya kipekee kwa wengi kushiriki kutembelea Kisiwa cha Saanane.

TANAPA imeendelea kuchukua hatua thabiti za kutangaza vivutio vya utalii wa ndani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kampeni kama hii ni sehemu ya juhudi za Shirika kuhakikisha Watanzania wanatambua na kufurahia urithi wa kipekee wa maliasili na mandhari nzuri zinazopatikana nchini.

Kampeni hiyo inatoa fursa kwa wapendanao kufurahia uzuri wa Hifadhi za Taifa kupitia vifurushi vya gharama nafuu vilivyoandaliwa mahsusi kwa msimu wa Sikukuu ya Wapendanao. Hifadhi zote 21 nchini zitashiriki, na wageni watapata nafasi ya kushuhudia maajabu ya maliasili na burudani za kipekee.

Wapenzi, familia, na marafiki wanahimizwa kutumia kipindi hiki kuungana na kusherehekea mapenzi yao katika moja ya vivutio vya kipekee vya Tanzania.