Kampuni ya gesi kuunga mkono juhudi za Serikali matumizi nishati safi kupikia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:03 PM Jan 24 2025
Kampuni ya gesi kuunga mkono juhudi za Serikali matumizi nishati safi kupikia.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kampuni ya gesi kuunga mkono juhudi za Serikali matumizi nishati safi kupikia.

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali ya kuimiza matumizi ya gesi safi ya kupikia, Kampuni ya Oryx Gas imeweka mikakati ya kufanikisha mpango huo kwa kutoa mitungi ya gesi na majiko yake kwa makundi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha mwaka 2025 cha  kampuni hiyo na mawakala wake kutoka mikoa yote nchini , Meneja Mauzo na Msimamizi wa Masoko wa kampuni hiyo nchini Tanzania, Shaban Fundi, amesema wanajivunia kuwa sehemu ya kufanikisha matumizi ya nishati safi nchini.

"Oryx Gas tumefika katika mikoa mingi sana tukihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na mwaka 2024 peke yake tumetoa mitungi ya gesi isiyopungua 39,000 kwa mpango Maalum wa kusaidia Kaya mbalimbali katika kijamii kwa kuwapatia mitungi ya gesi na majiko yake.

“Na wao wananchi wamekuwa mabalozi wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia na ukiangalia sio mwaka 2024 peke yake tumeanza tangu mwaka 2021 na ukiangalia tumetoa mitungi inayofikia 87000 mpaka sasa tena bure kabisa kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia

“Hii ni kwasababu tunaunga mkono juhudi za Serikali ambayo nayo imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati kupitia Wakala wa Umeme Vijijini(REA) tumeona wanahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,”amesema Fundi.

Ameongeza kuwa wao kama Oryx wataendelea kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na hiyo inawezekana kupitia Mawakala nchi nzima ambao wamekutana mwanzo wa mwaka 2025 kwa ajili ya kuweka mikakati ya kwenda kutekeleza mpango huo wa nishati safi ya kupikia nchini

Kuhusu mkutano wa mawakala wa Oryx Gas, Fundi amesema ni mkutano wao mkuu wa mwaka ambapo kampuni inaangalia utendaji wake wa mwaka 2024 na kupanga mikakati kwa mwaka 2025.

1

“Kwahiyo huu ni mkutano ambao unajumuisha mawakala wote nchi nzima ambao wako katika maeneo mbalimbali na sisi Oryx tunajivunia kuona tuna mawakala kila mkoa, kila wilaya pamoja na vijijini na ndio maana tunajidhatiti na kujipambanua kwamba tunauwezo wa kufikisha nishati safi ya kupikia katika maeneo yote nchini Tanzania ikiwemo na Zanzibar.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya hiyo upande wa  Zanzibar, Shuwekha Omar Khamis, amesema kukutana kwa mawakala hao kuna maana kubwa katika kuthibitisha dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kila mwaka wamekuwa wakikutana na kuangalia walikotoka na kuweka mipango mipya kufikia malengo yao.

Kuhusu matumizi ya nishati safi Zanzibar amesema kwa sasa yameongezeka kwani mwaka 2020 yalikuwa asilimia 7.7 ya usambazaji wa nishati safi  na mwaka 2024 yamefikia asilimia 26.5 na hiyo inamaanisha toka mwaka 2020 matumizi yao Zanzibar yametoka tani 3600  hadi kufikia tani 12400 mwaka 2024.

“Hii inatoa picha kuwa Wakazi wa Zanzibar wamebadilika, wameamka kutoka katika kutumia nishati chafu na kuingia katika nishati safi. Oryx Gas tumefanya jitihada kubwa katika kuwabadilisha wananchi wa Zanzibar kutoka katika nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwani tumechangia mitungi ya bure ambayo ni 18000 kwa mwaka 2024 

“Nawaomba wananchi wa Zanzibar waondokane na matumizi ya kuni na mkaa ambayo sio salama kwa afya yetu na mazingira.Wengi wetu tunapata madhara yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa na tunatumia gharama kubwa kujitibu.”Amesema
Shuwekha Omar Khamis.