ASKOFU wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza amechambua ushindi wa Tundu Lissu na kushindwa kwa Freeman Mbowe kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Juzi Kamati ya Uchaguzi wa CHADEMA ilimtangaza Lissu kuwa mshindi baada ya kupata kura 513 za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama sawa, akimwangusha Mbowe aliyekuwa anatetea kiti alichokikalia kwa miaka 21 na Odero Charles. Mbowe alipata kura 482 huku Odero akiambulia kura moja.
Kufuatia ushindi huo wa Lissu na timu iliyokuwa inamuunga mkono katika uchaguzi huo, akiwamo John Heche aliyemshinda Ezekia Wenje katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, Askofu Bagonza ameibuka na andishi lifuatalo:
---
Ninaandika kupongeza. Sina pole za kutoa.
Ninawapongeza Mwenyekiti Tundu Lissu na Makamu wake, mtani wangu Heche. Hata mimi siamini kama mmeshinda lakini sina pa kukata rufani. Mwaka huu nina bahati sana. Makamu wote wa vyama vikubwa ni watani wangu: Steven Wasira na Heche. Kuna nini hapa? Ninajiteua kuwa mpatanishi siku wakigombana.
Ninampongeza Freeman Mbowe. Ameshinda kuliko alivyoshindwa. Ametufundisha sote. Kukubali matokeo hutokana na mchakato uliojaa uhuru, uwazi na haki. Tuzo ya MO Ibrahim inamhusu lakini iwe na bahasha nzito, siyo kupewa ubao tu.
Ninampongeza Mwakajoka na Mnyika kwa kusimamia vizuri uchaguzi usiku kucha. Hakuna kazi mbaya kama kusimamia uchaguzi. Mwulizeni Mzee Lubuva! Baada ya pongezi, nibwabwaje haya:
1. Mbowe siyo Mugabe kwa sababu Mugabe hakuwahi kushinda wala kushindwa uchaguzi. Daima aliamua apate kura ngapi.
2. Mbowe siyo Mugabe wala wale wooote waliowahi kukaa madarakani muda mrefu. Nilikuwapo wakati wa JKN; kama angegombea 1985, angeshinda. Nilikuwapo mwishoni mwa Mzee Rukhsa, Mkapa, Kikwete, JPM (Atake Asitake), na hata sasa nipo na Mama, Chifu Hangaya. Wote hawa wangegombea baada ya vipindi vyao kwisha, bado wangeshinda! Mbowe ameshindwa na amekubali matokeo. Yeye ni zaidi ya “Bwawa Darasa” la siasa nchini.
3. Mbowe si Mugabe. Jamani! Si rahisi kumshinda aliye kitini. Mjinga mmoja wa chama kingine kaniandikia, “Mwamba kaamua tu kumlegezea mropokaji; angeamua kubaki wangemfanya nini?”
Nami nikamjibu, “waulize waliowahi kuamua kubaki. Toka kujadiliwa na Baraza la Mawaziri hadi kutojadiliwa na Baraza la Madiwani!” Huko si kuanguka ni kuporomoka. Mbowe kathibitisha umwamba wake.
4. Tundu Lissu siyo Trump. Wanafanana ukali wa maneno si ujinga wa kisiasa. Wote walipigwa risasi, zikawaongezea kura zao. Wapinzani wa Lissu ndani ya CDM wakapuuza risasi zake na kumwongezea huruma. Lissu ni hukumu isiyo na rufani kwa watawala wanaotumia risasi badala ya hoja. Rudisheni risasi mfukoni, nendeni shule mjifunze hoja. Wamarekani walitumia risasi, sasa wanaongozwa na “kichaa mstaarabu”.
5. Tundu Lissu siyo Trump. Kwa Trump mihimili inajitegemea na ina nguvu. Hapa kwetu, mihimili inamtegemea Lissu aiseemee na kuisimanga. Mmemsahau Spika Makinda? “Mwanangu Lissu, ebu tusaidie tuondoke hapo jamani”. Ninatamani Tulia atulie mbele ya Makinda apate twisheni ya kufanya kazi na Lissu.
6. Tundu Lissu na Freeman wameelewana. Wapambe wao wamenuniana. Tatizo lilikuwa moja. Tundu Lissu aliwamudu na kuwaendesha wapambe; Mwamba wapambe walimmudu na kumwendesha. Wote wawili ni somo kwetu: wapambe wanaweza kukuambia wakati gani kuingia uwanjani (Lissu), lakini hawawezi kukuambia wakati gani utoke uwanjani (Mwamba).
7. Mbowe amefuta makosa yake yooote ya miaka 21 kwa kubonyesha kitufe kimoja tu: kukubali matokeo. Lissu kachukua mkopo mkuuubwa wenye riba kubwa wakati kazungukwa na vibaka. Atamudu kurejesha mkopo huu? Neno kwa Mbowe: Ukistaafu, USTAAFU. Neno kwa Lissu: Mahaba ya kutongozea na kuolea ni tofauti na mahaba ya kuishi katika ndoa.
8. Wanachadema na Watanzania: Msiyemtaka kaja. Mliyemtaka kaja. Tuna taifa la kutunza na kustawisha. Mambo yetu hayako sawa. Walio madarakani wananung'unika. Walio nje wananung'unika. Wageni wananung'unika. Wawekezaji wananung'unika. Tusiridhiane ili hali iendelee. Turidhiane kuondoa hali hii. Watawala wa zamu, msipuuze watu kulala sakafuni Mlimani City. Kuna kitu ndani yao.
9. Wako wenye shaka na Lissu. Nami nimo. Tulio na shaka tuna bahati moja: hatuhitaji kumharibia Tundu Lissu. Yeye ana uwezo mkubwa wa kujiharibia. Tumwombee.
10. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa CCM kumaliza mkutano wake na CDM kuhitimisha uchaguzi wa ndani, taifa linaweza kuwa tayari limempata rais, chama tawala na chama kikuu cha upinzani. Penye CCM waweza kuweka CDM na penye CDM waweza kuweka CCM bila kuathiri maana ya nisemacho.
HAKI inaunganisha, DHULUMA inaligawa taifa.
Salaam nyingi toka barafu za milima ya Ufaransa na Ujerumani.
Ni mimi Lwakalinda Benson Kalikawe Bagonza
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED