Raia wa China, Tanzania kizimbani madai kukutwa na kobe 104

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 02:01 PM Jan 23 2025
Raia wa China, Tanzania  kizimbani madai kukutwa  na kobe 104.
Picha: Imani Nathaniel
Raia wa China, Tanzania kizimbani madai kukutwa na kobe 104.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewapandisha kizimbani raia wa China, Liang Zhou Liang (37), na raia wa Tanzania, Happyhania Chuoaza (31), wakikabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi kwa kukutwa na nyara za serikali, kobe 104, bila kibali.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo, wakili wa serikali, Tumaini Mafuru, alidai kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 16 mwaka huu katika eneo la Mwanzo Mgumu, Somangila, Kigamboni.

Kwa mujibu wa mashtaka, washitakiwa hao walikutwa wakimiliki nyara za serikali ambazo ni kobe 104 zenye thamani ya shilingi 18,022,950.40 bila kibali halali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washitakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili. Upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, lakini unakamilisha taratibu za kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuruhusu kesi hiyo kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi tarehe nyingine ambayo itapangwa kwa ajili ya kutajwa.