KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa kuimarisha ustawi na maendeleo ya Watanzania katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq wakati akihitimisha kikao cha Kamati hiyo na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bungeni jijini hapa juzi.
Kikao hicho kilikuwa maalum kwa ajili ya ofisi hiyo na taasisi zake kuwasilisha taarifa ya utendaji kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Disemba, mwaka jana.
“NSSF, OSHA, WCF na CMA kwa kweli kazi mnazofanya zinaonekana pamoja na changamoto chache zilizopo, sisi kama kamati tunaridhika na jinsi mnavyotekeleza majukumu yenu,” alisema na kuongeza kuwa:
“Kwa namna ya pekee nimpongeze Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake makini kwani tunatambua dhima kuu ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kunakua na ustawi na maendeleo ya Watanzania hususan wafanyakazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi.”
Mwenyekiti huyo wa kamati, alisema nia njema ya Rais Samia kuboresha ustawi wa wananchi wake inajidhihirisha katika jitihada ambazo serikali yake imekua ikichukua kuimarisha mifumo ya usimamizi wa masuala ya msingi, yakiwemo ya usalama na afya mahali pa kazi.
Aliupongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kufikia idadi kubwa ya maeneo ya kazi nchini na kuhakikisha wadau wanakua kuhusu usalama na afya kazini.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji majukumu ya ofisi hiyo, Waziri wa Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri Ridhiwani Kikwete, aliishukuru kamati hiyo kuishauri serikali kuhakikisha mipango yake ya maendeleo inafanikiwa.
Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema kupitia uwezeshaji wa serikali, wamejipanga kujiimarisha zaidi kiutendaji kwa kuongeza vitendea kazi, kujenga miundombinu bora ya kutolea huduma na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu masuala ya usalama na afya kazini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED