Serikali yaahidi kuimarisha ushirikiano na China

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 08:03 PM Jan 23 2025
Balozi wa China Nchini, Chen Mingjian.
Picha: Mpigapicha Wetu
Balozi wa China Nchini, Chen Mingjian.

SERIKALI imepigilia msumari dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na China katika sekta mbalimbali ili kuinua uchumi baina ya nchi hizo.

Hayo yalisemwa juzi jioni mkoani Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Methuselah Ntonda katika sherehe za mwaka mpya wa kichina.

Amesema sherehe ya mwaka mpya wa kichina imekuwa ikisherehekewa na maelfu ya raia wa nchi hiyo.

Aliongeza kwa sasa sherehe hizo zinafanywa hata na jamii za nje ya China kwa kuhusisha matukio ya kiutamaduni.

"Huu ni mwaka wa kitamaduni kwa wa China ambao aghalabu unapofika mwaka mpya huwa wanafanya sherehe kama hizo.Wameamua kufanya sherehe hizo Tanzania tangu miaka ya 80 wameona ni muhimu kushiriki tukio hilo na watanzania. Wanajivunia na watu wa Tanzania" alisema 

Vilevile aliipongeza serikali ya China kwa kusaidia nchi katika miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa Reli ya Kisasa, Uwanja wa Mkapa, na miradi mingine ya kimkakati.

Balozi wa China Nchini, Chen Mingjian alisema tukio hilo kwa watu wa china  ni kitu kikubwa na hutumika kama njia ya kujuliana hali, kula na kufurahi pamoja.

Alisema wapo baadhi ya wasanii kutoka China waliokuja kuungana na wenzao wa Tanzania kusheherekea sherehe hiyo.

"Tunataka kuchanganya hii furaha na Wachina wengi  wanaoishi Tanzania na tunafuraha pia kuona baadhi ya Watanzania wanapenda utamaduni wa kichina" alisema Balozi 

Alisema kufanyika kwa sherehe hiyo kwa amani nchini, ni ishara tosha kwamba nchi hizo ni marafiki akiahidi kuendelea kuudumisha udugu huo.

Katika sherehe hizo maelfu ya Wachina walifurika katika eneo la tukio kuungana pamoja kusherekea. 

Pia walikuwapo wasanii mbalimbali wa kichina walioeneza burudani katika ukumbi huo, jambo lililokuwa linaibua shangwe za maramara ukumbuni hapo.