AWAMU YA NNE: Ni zama za Lissu CHADEMA

By Restuta James , Nipashe
Published at 09:14 AM Jan 23 2025
 Ni zama za Lissu CHADEMA.
Picha: Nipashe Digital
Ni zama za Lissu CHADEMA.

BAADA ya timu zao za kampeni kutambiana kwa mwezi mmoja, hatimaye Tundu Lissu amekuwa Mwenyekiti wa nne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akimshinda Freeman Mbowe kwa tofauti ya kura 31.

Katika uchaguzi huo ulioanza juzi na kukamilika jana asubuhi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Lissu alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 513 sawa na asilimia 51.5 dhidi ya Mbowe aliyepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku mgombea mwingine Odero Charles akiambulia kura moja.

Akifunga Mkutano Mkuu wa chama hicho baada ya kutangazwa mshindi, Lissu alisema hatolipa kisasi kwa yeyote bali atahakikisha kila mmoja anapata haki.

“Tuna kazi ya kuwaambia wale waliofanyiwa kila aina ya vitimbi, walioenguliwa kwa njia za ajabu ajabu, tunahitaji kwenda kuwaambia tulifanya makosa, tunaomba msamaha sasa tuhakikishe kwamba haya mambo yaliyosababisha maumivu yote haya katika uchaguzi wetu hayajirudii tena. Si ya leo, na ya jana na juzi. Tutaenda huko tulikoanzia.

"Tutawarudisha wale waliokata tamaa, tutawapa tumaini jipya. Tutaombana msamaha, hatutalipizana visasi. Mimi ni mtu wa haki. Hatutalipiza kisasi, tutaponya wote walioumizwa," alisema.

"Na hili la juzi, hiyo chinjachinja ya wagombea nafasi za Kamati Kuu, hizi ambazo uchaguzi unafanywa Baraza Kuu, hayo maumivu tutaanza nayo. Wamekata rufani, tutazisikiliza kama zina haki, tutawarudisha," alisema.

Lissu pia alisema marekebisho ya katiba ya chama hicho yataweka ukomo kuwa awamu mbili pekee ili kiongozi aondoke madarakani kwa heshima.

"Mimi sitaki kuja kuhutubiwa kwamba ‘unajua umekaa hapa muda mrefu sana. Tutaweka ukomo na utaanza na mimi," alisema. "Tutaweka kwa umakini, hatutaweka kiholela ili kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo na mabadiliko. Tutaweka ili kuhakikisha hakuna ufalme na umalkia kwenye chama," alisema.

Kuhusu nafasi za viti maalum, Lissu alisema uongozi wake utaweka utaratibu wa kikatiba na kikanuni kuhakikisha kila mwanamke ambaye ni mwanachama wa CHADEMA, anapata haki sawa ya kugombea kwenye kata, majimbo na viti maalum.

Kuhusu ushauri aliopewa na Mbowe kuponya majeraha ya mchakato wa uchaguzi, Lissu alisema hayajaanzia kwenye uchaguzi mkuu bali kwenye ngazi mbalimbali.

Alisema uongozi wake utafanya kazi ya kujenga upya chama hicho kwa kuwa baadhi ya wagombea walienguliwa kwa mizengwe na figisu.

"Uchaguzi umeacha makovu mengi sana, makovu haya si ya jana wala juzi, yalianza tangu tulipoanza uchaguzi wa kanda. Watu wetu wameumizwa sana katika uchaguzi huo, tunahitaji kuwaponya," alisema Lissu.

Kuhusu fedha, Lissu alisema timu yake itatafuta fedha na kuzitumia kwa maslahi mapana ya chama hadi ngazi ya tawi.

Alisema kila ngazi ya uongozi itafanya kazi yake kwa uhuru, kinyume cha ilivyokuwa awali, maofisa wa makao makuu walikuwa wanahusika katika ngazi mbalimbali.

Lissu alisema kazi iliyoko mbele yao ni kudai mambo manne ambayo ni Katiba mpya, mifumo huru ya uchaguzi wenye tume huru na sheria bora za uchaguzi. Yasipopatikana hakutakuwa na uchaguzi.

"Tunakwenda kwenye uchaguzi tukiridhika kwamba ni uchaguzi wa kweli, hatutakwenda kwenye machinjio ya uchaguzi ambayo unajua kabisa unakwenda kuenguliwa," alisema huku akisisitiza uongozi wake utakabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatoingia katika mazungumzo ya maridhiano.

Makamu wake, John Heche alisema watafanya kazi usiku na mchana, kukijenga na kukikilinda chama hicho, akisisitiza "...tafsiri ya uchaguzi huu ni kwamba mtu yeyote asiye na ubini wa jina kubwa anaweza kuwa kiongozi mkubwa. Tunamshukuru sana Mbowe kwa kukijenga chama hiki, na sisi tutakilinda kwa ajili ya watanzania."

Jana jioni, kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Chama chini ya Mwenyekiti mpya Lissu kiliitishwa kwa ajili ya kupata wajumbe wanane wa Kamati Kuu, lakini uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na wagombea 19 kukata rufani kupinga kuenguliwa. 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, uchaguzi wa wajumbe hao utafanyika baada ya Kamati Kuu kuketi na kutoa uamuzi wa rufani zilizokatwa.