MWEZI ujao Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit), unaoandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO).
Ni mkutano uliopangwa kufanyika kati ya Februari 21 hadi 22, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo Dar es Salaam, huku kauli mbiu ya mkutano huo ikiwa ni “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.”
Katika mkutano huo, ambao mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, utahudhuriwa na Wakuu wa nchi zinazolima kahawa barani Afrika, mawaziri wa kilimo, sekta binafsi, viongozi wa taasisi za kahawa katika nchi zinazolima kahawa,wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao la kahawa.
Ni mkutano unaofanyika wiki nne, baada ya kufanyika tukio kubwa kama hilo kwa ngazi hiyo barani Afrika katika ukumbui huo tajwa, nao ukichukua siku mbili, wenyewe ukihusu sekta nishati, Rais Dk. Samia, naye akiwa mwenyeji wao.
Ni mkutano unaotarajiwa kutoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU), mashirika yake, benki za maendeleo za Afrika na taasisi nyinginezo za fedha, ili kuunda programu zinazochochea ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia sekta ya kahawa.
Katika Mkutano huo wa Tatu wa kahawa, kutajadiliwa maeneo muhimu katika mnyororo wa thamani wa kahawa, kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana katika maeneo mbalimbali.
Mkutano huo unaoshirikisha nchi 25 zinazolima kahawa Afrika, ni wa kuongeza ujuzi kuhusiana na zao hilo, kupata usahihi wa mnyororo wa thamani wa zao hilo.
WAZIRI WA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema utekelezaji kiserikali, umeshaanza kupitia wizara yake, wakizindua programu ya ujasiriamali kwa vijana iitwayo ‘Jenga Kesho Iliyo Bora’ (Build a Better Tomorrow – BBT).
Katika hilo, ina maudhui ya mipango inayotekelezwa ni kuanzisha wanachokiita “maduka ya kahawa yanayotembea,” kwa lengo la kuchochea na kuongeza matumizi ya kahawa nchini.
Bashe anasema, ni migahawa itakayowezesha vijana wajasiriamali kujiajiri katika maeneo mbalimbali, ikiwamo barabarani na kwenye matukio ya umma katika maisha ya kijamii.
Pia, Bashe anasema pindi mkutano huo utakapoisha, utawasaidia vijana kuanzisha vituo mahiri vya kuuza kahawa, kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, ili kuelimisha vijana mnyororo wa thamani wa kahawa, kutoka uzalishaji hadi matumizi.
Anafafanua, kuwa ni mpango unaoanzisha kikao cha wazalishaji kahawa Afrika, ni matokeo ya azimio lililopitishwa katika Mkutano wa 61 wa Mwaka wa IACO uliofanyika Kigali, Rwanda, Novemba 18, 2021.
Inatajwa ililenga kuandaa mkutano wa ngazi ya juu wa nchi 25 zinazozalisha kahawa Afrika, ili kutathmini mapungufu na changamoto zinazodumaza sekta hiyo katika ukanda huo.
Anasema, katika mkutano wa kwanza wa nchi hizo wazalishaji kahawa, ulifanyika nchini Kenya mnamo Mei 2022, ulipitisha kinachoitwa “Tamko la Nairobi"(Nairobi Declaration).
Hilo liliazimia kuweka mkakati wa kuingiza kahawa, kuwa bidhaa muhimu ya kimkakati ndani ya AU, sambamba na ajenda mwaka 2063 kwa AU.
Anasema mkutano wa pili wa nchi wazalishaji kahawa Afrika, ulifanyika Kampala, Uganda, Agosti mwaka 2023, ulipitisha tamko lililokusudia kuwaomba wakuu wa nchi 25 wazalisha kahawa kuunga mkono uidhinishaji kuwa bidhaa muhimu ya mkakati katika Ajenda ya AU mwaka 2063 na kuifanya IACO, kuwa shirika maalum la umoja huo.
Bashe anasema, katika kikao cha Baraza Kuu la AU, Februari mwaka jana huko Addis Ababa, wakuu wa nchi na serikali waliridhia ombi hilo; kahawa kuwa bidhaa muhimu katika mkakati na ajenda ya AU, mwaka 2063 ya AU, pia IACO kuwa shirika lake maalum.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NCHINI
Bashe anataja hatua zilizochukuliwa kutatua changamoto za biashara ya kahawa, baina ya nchi za Afrika, ni kuanzishwa Mkataba wa Biashara Huria Afrika (African Continental Free Trade Area - AfCFTA) wa mwaka 2018.
Anasema, lengo ni kuondoa vikwazo vya biashara katika nchi za Afrika, ili utekelezaji wa mkataba huo uimarishe biashara ya kahawa pasipo vizuizi.
USHIRIKI WA VIJANA
Carloline Samson, ni mjasiriamali mdogo, anataja faida kubwa ya mkutano ni jamii kujua umuhimu wa zao hilo la biashara na mnyororo wa thamani.
Anaipongeza serikali kwa kuandaa mkutano huo, akiamini utawaondolea kasoro ya ajira, hata wakajiajiri kupitia biashara ndogo za bidhaa hiyo, katika maeneo mbalimbali.
Anataja mkutano mkubwa wa ngazi hiyo, utawatambulisha wakulima wa kahawa wa nchini, pia kutatoa fursa kwa vijana kupata uzoefu kutoka kwa wakulima wakubwa wa zao hilo kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Caroline anasema serikali hivi sasa imewekeza katika sekta ya kilimo, hivyo mikutano mikubwa kama hiyo, inawasaidia kufungua fursa mbalimbali ambazo zinawasaidia vijana kujiinua kiuchumi wao wenyewe na familia zao.
Mjasiriamali huyo, anaishukuru Wizara ya Kilimo kwa ubunifu wa miradi itokanayo na sekta kilimo, ikiwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi, katika maeneo mbalimbali.
Mwigine ni Tito Mathiasa, anayesema kilimo cha sasa kinazidi kuhamia katika mapinduzi teknolojia, hivyo serikali kukubali kuandaa mkutano huo ni ya fursa ya kuwakutanisha wadau wa kahawa pamoja, kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu kilimo cha kahawa pamoja na mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Tito anaeleza kuwa, mkutano huo utatoa fursa nyingi kwa wakulima wa zao la kahawa, pia kupanua wigo wa kilimo cha kahawa nchini, ikiwamo kubadilishana mawazo wafanyabiashara na wazalishaji wa zao hilo la kahawa.
WADAU KILIMO KAHAWA
Mkulima Joshua Maganza, anasema mkutano huo ujao wa kahawa, utazidi kuitambulisha nchi kwenye kilimo hicho duniani, pia utazidi kuwashawishi wakulima kutanua wigo wa kilimo hicho nchini.
Anasema Wizara ya Kilimo, pamoja na serikali kwa ujumla, wako katika kukuza mazao ya kimkakati kama kahawa, jambo linalosaidia kuwashawishi wakulima kuongeza idadi ya ukubwa wa mashamba yao.
Anahimiza umuhimu wa zao la kahawa, pia kuwa la kimkakati, ambalo mkulima akifuata taratibu za kitaalamu za uandaaji wake, inapanua kiwango cha uzalishaji, hata kuongeza kipato cha familia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED